TANAPA YAKANA KATAVI KUUZWA

SHIRIKA la Hifadhi za Taifa (TANAPA), limekanusha taarifa zinazodai Hifadhi ya Taifa ya Katavi ipo kwenye mpango wa kukabidhiwa kwa wawekezaji kutoka nchini Afrika Kusini.

Habari hiyo iliandikwa Machi 25 mwaka huu na gazeti moja linalotoka mara moja kwa wiki ikiwa na kichwa cha habari kinachosema, "Nyalandu 'auza'Hifadhi".

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TANAPA kupitia Idara yake ya Mawasiliano, ilisema habari hiyo ilidai agizo la hifadhi hiyo kupewa wawekezaji, limetolewa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Bw. Lazaro Nyalandu Idara hiyo imeongeza kuwa, TANAPA ambayo ndio wasimamizi wa hifadhi hiyo na nyingine 15 nchi nzima, inakanusha habari hiyo na kudai imeandikwa kwa lengo la kupotosha umma.

"Hakuna mpango wala uamuzi wowote uliopo au uliofanywa wa kuingia mkataba wa uendeshaji hifadhi yoyote nchini kati ya TANAPA na mwekezaji yeyote kutoka nchini humo wala African Parks Network waliotajwa katika habari husika.

"Sheria inayosimamia uanzishwaji maeneo ya Hifadhiza Taifa ikiwemo Katavi, imelipa dhamana shirika kusimamia maeneo haya kwa niaba ya Watanzania hivyo ni kinyume cha sheria kukabidhi kwa wawekezaji kwa ajili ya usimamizi kama ilivyobainishwa katika habari hiyo," ilisema taarifa ya idara hiyo.

Iliongeza kuwa, TANAPA bado lina uwezo thabiti wa kusimamia uendeshaji wa hifadhi hiyo ili kuhakikisha rasilimali za wanyama na mimea zinaendelea kutunzwa kwa miaka mingi ijayo kama ambavyo imekuwa ikifanya tangu kuanzishwa kwa hifadhi husika 1974.

Taarifa hiyo ilisema shirika hilo limekuwa na mipango yake ya maendeleo mwaka hadi mwaka ambapo katika mwaka mpya wa fedha ujao, limepanga kuongeza idadi ya watalii katika Hifadhi za Kusini ikiwemo Katavi, Saadani, Mikumi na Ruaha.

Mkakati huo utahusisha kuongeza ubora wa utoaji huduma na malazi ili kukuza utalii wa ndani ambapo TANAPA itafungua ofisi jijini Dar es Salaam, kuimarisha Ofisi za Mwanza na Iringa ili watalii wapate taarifa za hifadhi."

Shirika litaendelea kujitangaza kupitia mitandao ya jamii, majarida, televisheni na kuiboresha tovuti ya shirika kwa kuwarifu wadau masuala mbalimbali yanayojiri kwenye hifadhi zetu.

"Tayari Shirika limeanzisha Kurugenzi mpya ya Utalii na Masoko kwa ajili ya kutekeleza mkakati wa kuzifanya hifadhi za Ukanda wa Kusini kuvutia watalii wengi zaidi," alisema.

Chanzo:Majira