Jaji Warioba ametoa rai hiyo jijini Dar es salaam baada ya kuzindua ripoti maalumu iliyotolewa na taasisi ya utafiti yatwaweza kuhusu katiba, ambapo amesema ili kuepuka hali inayoendelea katika bunge hilo, ni lazima wajumbe hao wafikie maridhiano kwani katiba haiwezi kupatikana bila ya kuwapo kwa muafaka baina yao.
Akizungumzia namna tume yake ilivyoshikamana katika kukusanya maoni ya wananchi jaji warioba amesema tume ilipata maoni kutoka kwa wananchi wanaozungumzia utawala bora, wanataka kuwapo kwa miiko ya uongozi, hivyo wakaa pamoja na kuyaratibu mwisho wa siku wakaja na rasimu moja, na kuwataka wajumbe hao wajirekebishe, wafanye kile ambacho wananchi wahitaji na kilichowapeleka Dodoma.
Uzinduzi huo pia umeshirikisha baadhi ya wajumbe wa bunge maalum la katiba ambapo Dk. Hamisi Kigangwala alikuwa miongoni mwao ambaye mbali na kutokukubaliana na utafiti huo kwa madai kuwa siyo wa kisayansi amesema kujitoa kwa baadhi ya wajumbe siyo sababu ya kuvunjika kwa bunge hilo bali litavunjika lenyewe hapo baadaye iwapo safu inayotakiwa kikanuni itapungua lakini akaongeza kuwa katiba haiwezi kupatikana bila kuwapo kwa maridhiano baina ya makundi yanayohusika.
Kwa upande wake Julius Mtatiro ambaye pia ni mjumbe wa bunge hilo amesema iwapo wajumbe wanataka kujadili muundo wa serikali mbili basi iundwe tume nyingine kwa ajili ya kujadili aina hiyo ya serikali na iwapo baadhi ya wajumbe hao wanang'ang'ania serikali mbili kitakachotokea ni wananchi kuendelea na katiba ile ile iliyopo na hivyo kukosa yale waliyoyataka kuingizwa kwenye katiba mpya kwa mustakabali wao.