KAMATI 6 ZA BUNGE LA KATIBA HAZIJAWASILISHA TAARIFA

KAMATI sita kati ya kamati 12 za Bunge Maalumu la Katiba, zimeshindwa kuwasilisha taarifa zao kwa Mwenyekiti wa Bunge Maalumu tayari kwa ajili ya kuwasilishwa bungeni leo.Jana, Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samia Suluhu Hassan, alipokea taarifa za kamati sita zilizomaliza kazi kwa wakati, huku kamati zingine zikiandika barua kuomba kuongezwa muda.Akizungumzia hali hiyo, Samia alisema kamati ambazo hazijakabidhi taarifa zao, zitaendelea kukabidhi taarifa hizo leo wakati zilizowahi kuwasilisha taarifa zao mbele ya Bunge Maalumu.

Alisema taarifa za kamati zilizokwisha wasilishwa, zitatolewa nakala ili kazi ya kuwasilishwa ndani ya Bunge leo iendelee wakati kamati zilizochelewa, zikiendelea kuwasilisha taarifa zao.

Samia pia alibainisha kuwa Kamati ya Uongozi iliyoanza kikao chao jana saa mbili usiku, ilitarajiwa kutoa ratiba kamili leo kuhusu kitakachofuata katika Bunge Maalumu.

Waliokabidhi Kamati ya Kwanza kuwasilisha taarifa yake ni Kamati Namba Tisa inayoongozwa na Mwenyekiti Kidawa Hamidi Saleh na Makamu Mwenyekiti, Wiliam Ngeleja na kufuatiwa na Kamati Namba Tano, inayoongozwa na Mwenyekiti Hamad Rashid Mohamed na Makamu Mwenyekiti, Assumpter Mshama.

Kamati zilizofuata ambazo ziliwasilisha jana saa 10 jioni ni pamoja na Kamati Namba Mbili, inayoongozwa na Mwenyekiti Shamsi Vuai Nahodha na Makamu wake, Shamsa Mwangunga na Kamati Namba 11, inayoongozwa Mwenyekiti Anne Kilango Malecelana Makamu Mwenyekiti, Hamad Masauni.

Kamati ya tano kuwasilisha taarifa yake kwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu ni Kamati Namba 12, inayoongozwa na Mwenyekiti Paul Kimiti na Makamu Mwenyekiti, Thuwaybah Kisasi na Kamati Namba 10, inayoongozwa na Mwenyekiti Anna Abdallah na Makamu Mwenyekiti, Salmin Awadh Salmin, ilikuwa ya mwisho kuwasilisha taarifa zake.

Theluthi mbili Ukiacha Kamati Namba Tisa inayoongozwa na Mwenyekiti Kidawa, ambayo imepata theluthi mbili katika kila ibara ya sura ya kwanza na sura ya sita za Rasimu ya Katiba mpya, kamati zingine tano hakuna hata moja iliyopata theluthi mbili katika ibara zote.

Nahodha katika taarifa yake, alisema katika kamati yake katika Sura ya Kwanza, hawakupata theluthi mbili ya kura zote katika ibara ya kwanza na ibara ya nane kifungu kidogo cha nne.

Anne Kilango katika taarifa yake, alisema walifanya kazi mpaka usikuna katika Sura ya Kwanza, walipata theluthi mbili ya kura za Tanzania Bara, lakini Zanzibar hawakupata.

Anna Abdallah alisema muda haukutosha na katika majadiliano, misimamo ya vyama vya siasa ilionekana wazi na hivyo hata katika kuamua kwa kura ni mambomachache, ndiyo walipata theluthi mbili ya kura kutoka Tanzania Barana Zanzibar.