TIMU YA TANZANIA CHINI YA MIAKA 20 YASONGA MBELE

Timu ya taifa ya soka ya Tanzania kwa vijana wenye umri wa miaka 20 imesonga mbele kwenye safari ya kufuzu kwa Fainali za Kombe la mataifa baada ya kuilaza Kenya kwa mikwaju ya Penalti 4-3 kwenye mechi ya marudiano iliyochezwa kwenye uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam.

Mechi hiyo imelazimika kuingia hatua ya Penalti baada ya kumalizika dakika 90 mechi ikiwa sare ya 0-0 nandipo Tanzania ilipopata ushindi unaoisogeza kwenye raundi ya pili ya michuano hiyo inayofanyika kila baada ya miaka miwili.

Ushindi huo wa timu ya Tanzania ijulikanayo kana Ngorongoro Heroes umekuwa faraja kwa Watanzania baada ya timu yaTaifa ya wakubwa, Taifa Starskuchezea kichapo dhidi ya Intamba Murugamba ya Burundi Jumamosi kwenye mechi ya kirafiki ya maadhimisho ya miaka hamsini ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambapo Taifa Stars ilichapwa mabao 3-0.

Nalo Shirikisho la soka nchini Tanzania TFF limemtangaza rasmi kocha mkuu mpya wa timu ya taifa ya soka ya Tanzania Taifa Stars Martinus Ignatius Nooij ambaye amesaini mkataba wa miaka miwili kuionoa timu hiyo huku kibarua chake cha kwanza kikiwa tayari kimeishatangazwa ambapo Taifa Stars itashuka dimbani dhidi ya Zimbabwe mwezi Mei mwaka huu kwa mechi ya awali ya kufuzu kwa Fainali za Kombe la Mataifa zitakazofanyika mwakani nchini Morocco mwezi Februari mwakani.

Tayari Kocha ametangaza majina ya wachezaji tisa wapya kuimarisha kikosi hicho huku beki maarufu wa timu ya Yanga, Kelvin Yondan akitemwa kwenye kikosi hicho baada ya kugoma kuripoti kambini, pasipo kutoa sababu za msingi za kutofanya hivyo.


Katika safari ya kuelekea Morocco hapo mwakani, Uganda itashuka dhimbani dhidi ya Madagascar, huku Burundi ikicheza dhidi ya Botswana, na Harambee Starsya Kenya itapepetana na Commoro, nayo Rwanda ikicheza dhidi ya Libya.