KINGUNGE AWATAKA KUFYATE WANAO MSHAMBULIA JAJI WARIOBA

Wajumbe wa Bunge Maalum wametakiwa waache kumsakama aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Mstaafu Joseph Warioba na timu yake, kwani maoni alowasilisha si yake, bali ni ya wananchi.

Rai hiyo imetolewa Bungeni hapa leo na Mwanasiasa Mkongwe, MzeeKingunge Ngombale-Mwiru wakati akitathmini mwenendo wa Bunge hilo katika mjadala wa Rasimu ya Pili ya Katiba.


Mzee Ngombale-Mwiru amewatahadharisha wajumbe wasivuke mipaka, akiwaeleza hawakwenda Dodoma kuipiga vijembe timu ya Warioba, bali wana wajibu wa kuhakiki na kuboresha Rasimu ya Katiba Mpya.


"Kero ya wananchi kubwa kabisa ni kero ya umasikini," amekumbusha Kingunge, akiliambia Bunge kuwa wana wajibu wa kuhakikisha Katiba wanayoandika inaakisi matatizo haya na inazungumzia "hatma ya wananchi."

Huku hayo yakiendelea, Waziri Mkuu Mizengo Pinda amewataka wajumbe wa Ukawa walosusia vikao warejee Bungeni hapa, na wamalize tofauti zao ili Katiba ya Wananchi ipatikane.


Bunge hilo limeahirishwa hadi Agosti 05 mwaka huu, litakapokutana tena mjini hapa kwa miezi miwili ili kuhitimisha kazi waliyoianza ya kuandaa Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.