MENEJA BARCLAYS MBARONI KWA WIZI

POLISI Kanda Maalumu ya Dar es Salaam inawashikilia watuhumiwa 13, wakiwamo mameneja wawili waBenki ya Barclays kwa tuhuma za kuhusika na wizi katika benki hiyo katika tawi la Kinondoni. Mameneja hao ni Alune Kasililika maarufu kama Mollel (28), mkazi wa Kimara Bonyokwa ambaye ni Meneja wa tawi hilo na Neema Bandari maarufu kama Bachu (28) ambaye ni Meneja Operesheni wa tawi hilo.

Kamishna wa Kanda hiyo, Suleiman Kova aliwaambia waandishi wa habari kuwa watuhumiwa hao wanahusishwa katika ujambazi uliotokea Aprili 15, mwaka huu saa 3:30 asubuhi.Alidai katika siku ya tukio hilo, watuwenye silaha aina ya SMG na bastola waliingia katika benki hiyo na kupora Sh milioni 390.22, dola za Marekani 55,000, Euro 2,150 na Pauni 50.

"Majambazi hao waliwatishia kwa silaha watumishi wa benki hiyo na kuwaweka chini ya ulinzi na hatimaye kutoroka na fedha hizo kwa kutumia pikipiki aina ya Fekon," alisema. Alidai awali watuhumiwa hao walifika katika benki hiyo wakiwa na magari mawilimoja aina ya Opa lenye namba T421 BQV ambayo imekamatwa.


Kwa mujibu wa madai ya Kova, uchunguzi wa kina ulibaini kuwa Alune alishirikiana na Neema pamoja na watuhumiwa wengine kufanikisha tukio hilo, huku ikigundulika kuwa robo tatu ya fedha zote zilizoibwa zilichukuliwa kabla ya tukio hilo.

"Siku hiyo ya tukio ilikuwa ni utekelezaji ili kukamilisha njama zao, hawa walisakwa na vikosi mbalimbali maalumu ikiwa ni pamoja na Kikosi Maalumu ambacho ni kwa ajili ya kuzuia na kupambana na wizi katika mabenki jijini Dar es Salaam," alisema.


Aliwataja watuhumiwa wengine kuwa ni Fredrick Lazaro (19), Kakamiye Julius (31), Iddi Nguvu (32), Sezary Massawe maarufu kama Msolopa, Boniface Ndaro maarufu kama Muumba (29), Erasmus Mroto maarufu kama Menyee (38), Deo Olomy (32), Mohamed Athumani (31), Joseph Mkoi (33), Lucy Amos maarufu kama Macha (30) na Grace Amon (39).


Alisema baada ya watuhumiwa hao kuhojiwa, baadhi yao wamekiri kuhusika na wizi huo na walipopekuliwa walikutwa na fedha kidogo ambazo ni sehemu ya mgawo waliopata baada ya tukio hilo."


Kabla ya tukio lile, imebainika kulikuwa na vikao mbalimbali vya maandalizi ya kufanikisha tukio hilo kabla ya siku hiyo.

"Matukio kama haya yanatudhalilisha, yanatoa picha kwamba Jeshi la Polisi na serikali tumeshindwa kuzuia uhalifu wa ainahii lakini kumbe ni kazi iliyofanyika ndani," alisema Kamanda Kova.

Alisema bado upelelezi unaendelea, hivyo wananchi waendelee kushirikiana na Polisi ili watuhumiwa wengine wakamatwe na sheria ichukue mkondo wake.

Katika hatua nyingine, Kova alisema kwa sasa wataanza kuwachukulia hatua wamiliki wa hoteli zenye mabwawa ya kuogelea ambayo hayana uangalizi wakati watu wakiogelea.


Hatua hiyo inatokana na tukio la watoto watatu kufa wakati wakiogelea katika bwawa la kuogelea kwenye Hoteli ya Landmark iliyopo Mbezi Jangwani, tukio ambalo ni la juzi saa 11:00 jioni.


Alisema mtoa taarifa David Mboka (44) alisema akiwa hotelini hapo kusherehekea siku ya kuzaliwa ya mtoto wake, Derrick Mboka (1) aligundua watoto hao ambao ni Ndimbuni Bahati (9), Eva Nicholous (9) na Janeth Zacharia (10) wametumbukia katika bwawa hilo.


"Matukio ya aina hii tunaanza kuyafanyia kazi na tunaanza na huyu, pia tunatoa onyo kwa wamiliki wengine ambao wana mabwawa ya kuogelea kuwa makini na maeneo hayo kwa kutoruhusu watoto kukaribia maeneo hayo," alisema Kova.