AJINYONGA BAADA YA KUMKUMBUKA MKEWE

MKAZI wa Mtoni Kijichi, Richard Kijazi (36) amekutwa amekufa kwa kujinyonga chooni na kuacha ujumbe kwamba amejiua kwa sababu ya kumkumbuka marehemu mkewe.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Engelbert Kiondo, alisema jana kuwa Kijazi alijiua juzi saa 11:15 jioni katika maeneo ya Mtoni Kijichi, Wilaya ya Temeke.

Alisema Kijazi alikutwa amejinyonga kwa kutumia kitambaa cha nguo alichokitundika kwenye kenchi ya choo ya nyumba anayoishi.

Ujumbe uliokutwa katika eneo hilo ulisomeka:

"Hajahusika mtu yeyote kuhusu hili, nimemmiss Mama John wangu, nizikwe Dar es Salaam na Mchungaji Haule naomba ujumbe huu uheshimiwe."

Kwa mujibu wa Kamanda Kiondo, uchunguzi wa awali umebaini kuwa Mama John alifariki mwaka 2012 baada ya kuugua malaria na tangu wakati huo Kijazi alikuwa akijaribu kujiua na kuokolewa na ndugu zake.


Maiti amehifadhiwa katika Hospitaliya Temeke. Katika tukio jingine, Kamanda Kiondo alisema, Mwendesha Pikipiki, Said Jongo (32)amekufa papo hapo baada ya kugongwa kwa nyuma na gari aina ya Toyota Coaster lenye namba T412 ATJ.


Ajali hiyo ilitokea juzi saa 12:00 jioni katika Barabara ya Chamazi eneo la Charambe Magengeni, ambapo gari hilo likiendeshwa na mtu asiyefahamika akitoka Mabagala Rangi Tatu kwenda Chamazi, liligonga kwa nyuma pikipiki yenye namba T281 CKY ainaya Fekon, iliyokuwa ikiendeshwa na Jongo.

Mwili wa Jongo umehifadhiwa katika Hospitali ya Temeke na dereva wa gari hilo aliyekimbia baada ya ajali bado anatafutwa, gari liko katika Kituo cha Polisi Mbagala.


Katika tukio la tatu, mkazi wa Majohe aliyetambuliwa kwa jina la Erasmus Marshal (52), amekutwa amekufa chumbani kwake huku mwili ukiwa umeanza kuharibika.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi, alisema mwili wa Minangi ulikutwa juzi saa 7:00 mchana huko Majohe Kichangani ukiwa umekaa kitandani huku umefunikwa shuka na mezani kwake kulikutwa mabaki ya chakula aina ya utumbo na soda ya Azam Malta.


Uchunguzi wa awali kwa mujibu wa Kamanda Minangi, umeonesha kuwa enzi za uhai wake alikuwa akiishi peke yake kwenye nyumba hiyo na mwili wake umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa uchunguzi zaidi.