Hivyo ndivyo ilivyokuwa mapema asubuhi hii ya leo, wakati kuta za barabara ya inayounganisha kati ya jiji la Dar-es-salaam na Bagamoyo mkoa wa Pwani, lilivyokuwa likimomonyoka kadri mvua zilivyokuwa zikiendelea kunyesha katika eneo hilo la Bunju Mpiji mpakani mwa Bagamoyo na jiji la Dar-es-salaam.
Akiongea na wananchi waliokuwa wamefurika katika eneo hilo, waliokuwa wanahitaji kusafiri kati ya Bagamoyo mkoani Pwani na Dar-es-salaam, waziri wa ujenzi Mheshimiwa John Pombe Magufuri, aliyefika katika eneo hilo ili kushuhudia kadhia hiyo ya mvua na kutoa kauli ya serikali amesema kuwa, tayari amewasiliana na jeshi la wananchi Tanzania (JWTZ) ili kupata madaraja ya muda huku zaidi maroli elfu moja ya mawe yakihitajika kujazwa eneo hilo ili kuruhusu magari na watu kuweza kupita katika eneo hilo.
Mkuu wa mkoa wa Dar-es-Salaam bwana Saidi Mecki Sadik aliyeambatana na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wa Dar-es-Salaam, amesema kuwa mpaka sasa jiji la Dar-es-Salaam limepoteza watu wa nane kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha jijini, huku akisisitiza kuwa, uhamaji wa mito na kuharibu kingo za madaraja jijini Dar-es-Salaam, zinatokana na shughuli za kibinadamu ikiwemo uchimbaji holela wa mchanga na kulima karibu na mito.
Baadhi ya wanafunzi mbalimbali waliokuwa wakitoka jijini Dar-es-Salaam na wale waliokuwa wakitoka mashuleni, mara baada ya shule kufungwa kwa wiki moja, ili kupisha mapumziko ya sikukuu za pasaka, wamejikuta wakilazimika kuzungukia njia mbadala za bunju, Goba kutokea na kuingilia Boababu ili kupata mawasiliano kati ya Bagamoyo na Dar-es-salaam.
katika eneo hilo la tukio, tingatinga na askari wa jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ) tayari walikuwa katika eneo hilo la tuko ili kuweza kurejesha mawasiliano ya barabara hiyo huku jeshi la polisi kanda maalumu ya Dar-es-salaam na wale wa Bagamoyo mkoa wa Pwani wakiimalisha ulinzi katika eneo hilo.