KENYA YAWARUDISHA WASOMALI KWAO

Serikali ya Kenya imewarudisha nyumbani Wasomali 82 waliokuwa miongoni mwa wageni3000 walioshikwa katika msako mkubwa unaoendelea mjini Nairobi kukabiliana na tishio la ugaidi.

Mwandishi wa BBC mjini Nairobi, Paul Nabiswa, ambaye yuko katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta ameshuhudia zaidi ya Wasomali 82 wakiingizwa katika ndege moja ambayo imekodishwa maalum kwa shughuli hiyo.

Balozi wa Somalia nchini Kenya , Mohammed Nur amesema kuwa ndege hiyo imekodishwa na serikali ya Somalia baada ya watu hao kuamua kwa hiari yao wenyewe kurejea nyumbani baada ya kukamatwa katika msako unaoendelea mjini Nairobi wakiwa hawana vibali rasmi ya kuishi nchini Kenya.

Balozi huyo anasisitiza kuwa wasomali wengi wakimbizi walionaswa wakiwa na stakabadhi rasmi za Shirika la umoja wa mataifa linaloshughulikia wakimbizi UNHCR wataregeshwa katika kambi za wakimbizi baada ya uchunguzi wa serikali ya Kenya.

Msako huu unaoendelea sasa mjini Nairobi ulianza ijumaa iliyopita baada ya kutokea milipuko ya grenadi mtaani Eastleigh.

Watu sita waliuawa katika matukio hayo ya mwisho yaliyoibua hasira miongoni mwa wakenya na kuchochea serikali kuanzisha msako huu.

Kufikia jana Polisi ya Kenya ilidhibitisha kuwa imewanasa wahamiaji 3,000 na kuwaachilia huku ikiwa imesalia na wahamiaji 447.