MIRUNGI YA VIDONGE YATEKA WATANZANIA

Unapolitaja neno 'mirungi' macho na hisia zako zitakupeleka katika dawa zakulevya zilizo katika mfumo wa majani au mimea ambazo ni maarufu Afrika Mashariki. Hapa nchini mirungi imeharamishwa kulingana na sheria ya dawa za kulevya.

Hata hivyo kwa sasa, mirungi hii haitumiwi ikiwa katika hali ya mimea tu kama ilivyozoeleka bali katika mfumo wa kidonge (kitaalamu synthetic cathinone) ambacho ni vigumu kufahamu kama ni mrungi.

Dawa hii ya kulevya ni maarufu na ina majina mengi hapa duniani, baadhi ya majina hayo ni miraa, khat kwa Kiingereza, ghat, qat, hagat, bushman tree (Afrika Kusini) na baadhi wanauita mmea huu Arabian.

Imebainika kuwa mirungi ya vidonge huingizwa nchinikatika vifurushi vilivyobandikwa lebo kama vile dawa za kuua wadudu, bath salt, sumu kali, dawa za kusafishia vioo au simu na mimea.

Mwaka 1980, Shirika la Afya Duniani liliipanga mirungi kuwa katika kundi la dawa za kulevya na mihadarati inayosababisha utegemezi, wakati hapa nchini mirungi ilipigwa marufuku Aprili 1991.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Akili na mshauri wa watumiaji wa dawa za kulevya, Innocent Godman, alifanya utafiti mwaka 2004 kuhusu utumiaji wa mirungi hapa nchini, ambao ulibaini kuwa kuna ongezeko kubwa la watumiaji wa mirungi ya kidonge.

"Ingawa mirungi ya vidonge imeanza kutumika katika siku za karibuni, lakini mirungi ya mimea, ilianza kutumiwa miaka 800 iliyopita," anasema Dk. Godman.

Mirungi ya kidonge inatajwa kuwa na madhara makubwa kuliko ile ya mimea, kwani husababisha mtumiaji kupata raha ya ngono au kilele cha mapenzi kwa sekunde 17 tofauti na hali ya kawaida ambapo binadamu hupata kilele hicho kwa sekunde tatu tu.

"Kidonge cha mirungi kimekuwa maarufu zaidi kwa sababu mtumiaji hupata raha ya mapenzi kwa muda mrefu na hivyo kumfanya asiwe na sababu ya kuwa na mwenza," anasema na kuongeza:

"Mirungi hii ina kileo kinachoitwa 'cathinone' mbacho ni kichocheo kinachobadilisha kasi ya ufanisi wa ubongo. Kinasogeza mbele uchovu, njaa na kuongeza umakini. Kikubwa zaidi kileo hicho husababisha raha ya ngono (euphoria) kudumu kwa muda mrefu."

Dk. Godman anasema, matumizi ya kidonge cha mirungi hapo zamani yalizoeleka zaidi kwa watu wazima wenye umri wa miaka 50 na kuendelea wenye matatizo ya nguvu za kiume, lakini hivi sasa, vijana wadogo wanatumia vidonge hivyo.

Katika utafiti huo ilibainika kuwa watumiaji wa mirungi hupenda kutembelea maeneo maalumu kwa mfano Dodoma, ni karibu na soko kuu na Arusha, ni maeneo ya Ngaramtoni, Makao Mapya na Kaloleni.

Lakini yapo maeneo maarufu katika Jiji la Arushana Dar es Salaam yanayoitwa Manjili Sairat ambayo yanasifika kwa kuuza mirungi ya majani na kidonge.

Mirungi ya kidonge kwa kawaida humezwa au mtumiaji kujidunga kama watumiaji wa dawa za kulevyawanavyojidunga, kukichanganya kwenye chai, lakini baadhi hukiingiza katika njia ya haja kubwaau (booty bombing).Matumizi ya mirungi licha ya kutopewa uzito mkubwa hapa nchini, lakini imebainika kuwa inatumiwa na watu zaidi ya milioni 10.Kamishna wa Kitengo cha Kupambana na dawa za Kulevya, nchini, Alfred Nzowa, anasema hana taarifa za kuwepo kwa mirungi ya vidonge zaidi ya mirungi ya majani.Hata hivyo Nzowa anasema, watatafuta mirungi na watapeleka sampuli kwa mkemia mkuu ili kujua madhara zaidi na iwapo wanachanganya na vitu vingine."Kikosi kazi changu kitaisaka mirungi hiyo kwa namna yeyote ilewanayoifungasha na tutaipima, ingawa kisheria tangu zamani mirungi haikubaliki hapa nchini," anasema Afande Nzowa.

*Waganga wa jadi nao wamo

Pia matumizi hayo yameenda mbali zaidi ambao hata waganga wajadi wanatumia mirungi ya majani kama dawa ya kifafa, kuongeza nguvu za kiume, kutibu maradhi ya pumu na dawa za kuongeza bahati.

"Kwa baadhi ya tamaduni, iliaminika mtu kuweka jani la mrungi katika mfuko au wanawake kulifutika katika maziwa, wakati anapokwenda kufanya biashara, kunaleta bahati,"anasema.

Si hivyo tu, kwani zipo baadhi ya nchi zimeruhusu wakazi wake kutumia mirungi kama mmea unaosaidia kuondoa usingizi na uchovu, hivyo wanafunzi, madereva na madaktari wamekuwa wakiutumia ili kupoteza usingizi.

Kamishna Msaidizi Tume ya Kupambana na Dawa za Kulevya, Aida Tesha pia hafahamu uwepo wamirungi ya vidonge.

"Tutaliwasilisha hilo jambo mbele ya wenzetu na kuanza kulifanyia utafiti, kwangu hii ni habari mpya kabisa," anasema.

Utafiti wa Dk. Godman unaonyesha kuwa watumiaji wa mirungi hasa ule wa kidonge wametofautiana kimadaraja kwa mfano, watumiaji wa mirungi walioajiriwa ni asilimia 59, wakati ambao hawaja ajiriwa ni asilimia 11 na wanafunzi ni asilimia tisa.

Makundi mengine ya watumiaji wa mirungi yalichambuliwa na kuonekana kuwa ambao hawana wenza ni asilimia 30, waliooa ni asilimia 60 na waliochana ni asilimia 10 wakati wajane ni asilimia 10.

*Madhara ya kiafya ya mirungi

Mirungi (ya mimea na ya kidonge) ina madhara ya kifikizia na kitegemezi kama ilivyo mihadarati mingine.

Kwa mfano mtumiaji huweza kutanuka mboni ya jicho lake, ndoto mbaya usiku, msonono, ongezeko la kasi la damu, kukosa hamu ya kula, na kuongezeka kwa kiwango cha raha ya tendo la ndoa.

Yapo matokeo ya papo kwa papo yakutumia mirungi ambayo ni pamoja shinikizo la damu, kukosa uhalisia wa dunia(kujihis tajiri, mwenye pesa au upo nchi za Ulaya) kitaalamu ni Cycosis.

Madhara yanayoweza kumpata mtumiaji baada ya kipindi kirefu ni pamoja na wazimu, maradhi ya saratani hasa ya mdomo, kiharusi, kuziba kwa mishipa ya damu ya moyo na kuharibika kwa ini.