Taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa TMA, Dk Agness Kijazi ilisema kiwango cha uhakika wa kuwapo kwa matukio hayo ni kwa asilimia 70.
Alisema matukio hayo yameanza Aprili 11, mwaka huu na yataendelea hadi 14 mwaka huu.
Alisema kutakuwepo na vipindi vyamvua kubwa inayozidi milimita 50 ndani ya saa 24, upepo mkali unaozidi kilometa 40 kwa saa na mawimbi makubwa, yanayofikia mita mbili katika ukanda wa pwani.
Alitaja maeneo yanayotarajia kuathirika kuwa ni Visiwa vya Unguja na Pemba, mikoa ya Dar esSalaam, Pwani, Tanga.
Kuna uwezekano mikoa ya Lindi, Mtwara na Morogoro nayo itaathirika na hali hiyo.
Dk Kijazi alisema hali hiyo, inatokana na kuimarika zaidi kwa ukanda wa mvua wa 'Inter-tropical Convergence Zone (ITCZ)', ambao umeambata na na ongezeko la unyevunyevu katika eneo la Bahariya Hindi.
Alionya wakazi wa maeneo hatarishi, watumiaji wa bahari na mamlaka zinazohusika na maafa, kuchukua tahadhari zinazotakiwa, kutokana na hali hiyo.
Alisema kwamba mamlaka hiyo inaendelea kufuatilia hali hiyo na itatoa taarifa kila itakapobidi.