Katika tukio hilo askari polisi Koplo Mohammed Mjombo(44) aliuawa huku mwenzake mwenye namba Konstebo Ibrahim Juma Mohammed(35) akijeruhiwa vibaya kwa risasi kabla ya kuporwa silaha aliyokuwa nayo.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Mkurugenzi wa Upelelezi Zanzibar, SACP Yusufu Ilembo amesema kuwa pamoja na kukamatwa kwa silaha hizo pia watuhumiwa watatu kati ya wanne waliohusika katika mauaji ya Polisi wamedakwa.
Alisema silaha hizo zilikamatwa nyumbani kwa mmoja wa watuhumiwa anayeishi eneo la Mkokotoni katika mkoa wa Kaskazini Unguja zikiwa zimefungwa na vipande vya plastikina vitambaa na kuviringishwa katika waya mpya wa kupigilia madirisha.
Bila ya kuwataja majina yao kwa sababu za kiupelelezi, DCI Ilembo ameainisha wazi kuwa baadhi ya watuhumiwa hao ni wenyeji wa Pangani mkoani Tanga na wengine ni wenyeji wa Kisiwa cha Pemba Zanzibar.
Amesema katika mahojiano na makachero wa Polisi, Majambazi hayo pia yalikiri kuhusika na matukio mbalimbali katika mikoa ya Visiwani na Mikoa ya Tanzania Bara matukio ambayo yangali yakichunguzwa katika Vituo mbalimbali vya Polisi.
Watuhumiwa hao pia walipatikana na vitu mbalimbali zikiwemo fedha taslimu shilingi 490,000 za Kitanzania, dola 75 za Kimarekani, Euro na fedha kadhaa za Kichina pamoja na vitu mbalimbali zikiwemo simu za mkononi.