Akizungumza kwenye Viwanja vya Bunge mjini hapa mara baada ya nakala kugawiwa bungeni, Lissu ambaye aliibua hoja hiyo alisema; "Hivi hawa wanamghiribu nani? Nasema hiyo hati haikuwahi hata kupelekwa Umoja wa Mataifa."
Alisema saini iliyo kwenye hati hiyoni tofauti na zilizo kwenye hati ya Mabadiliko ya Kwanza ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya 10 ya Juni 1965, Hati ya Muswada wa Sheria ya Udhibiti wa Fedha za kigeni na Sheria ya kugawa ardhi kwa Wazanzibari ambazo zote zinafanana.
Lissu alisema kwa miaka 50 haikuwahi kuonyeshwa, wala haikuwahi kuwa UN na hata Zanzibar hawana.
Alisema walishuhudia Benard Membe (Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa) akisema iko UN, jambo alilosema ni kudanganyana tu.
Alisema nyaraka kama hizo, mkataba wa Uhuru zinatakiwa kuwekwa Makumbusho ya Taifa kwa kuwa ni nyaraka wazi zinazotakiwa kuona na kila anayetaka, kwa rahisi.
"Marekani ilipata uhuru zaidi ya miaka 200, lakini kila nyaraka za uhuru zinaonekana kwa rahisi siyo hapa...mambo yanafanyika chini kwa chini, utadhani biashara haramu," alisema.
Baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu wamembeza Lissu kwa hoja hiyo wakisema hatua ya nakalazake kufikishwa bungeni ni sawa na kumfunga bao la kisigino na kuhoji watazungumza nini baada ya hati kupatikana.