Kutokana na hali hiyo, Kiongozi huyo, amesema chama chake kamwe hakitowavumilia watendaji wanaoendekeza vitendo vya urasimu na umangimeza wa kutumia makaratasi ofisini badala ya kuwatumikia wananchi kwa kuwajibika ipasavyo.
Akizungumza mara baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa gati ya bandari ya Kirema na baadaye katika mkutano wa hadhara walayani hapo, alisema ni jambo laaibu kwa watendaji wa Serikali kumuachia mkandarasi asiye na sifa miradi muhimu kwa muda wa miaka mitatu bilo kufuatilia utendaji wake.
Mkandarasi huyo wa Modispan Enterprises Limited, pamoja na mradi huo wa ujenzi wa gati katika bandari hiyo ya Karema ambayo thamani yake ya ujenzi ni Sh bilioni 1.5, pia anajenga gati katika bandari za Mwangosa, Sibwete na Lupili.
Alisema atahakikisha analifikisha suala hilo katika vikao vya juu na kulivalia njuga ili kubaini mkandarasi huyo ni nani, alipataje zabuni hiyo na akina nani walihusika kumpatia na kwanini hadi leo hajachukuliwa hatua za kunyang'anywa miradi hiyo isiyoendelea.
Pamoja na suala hilo la bandari pia Kinana alitembelea mradi wa ujenzi wa Mwani ambao utatumika kama soko na eneo la kuhifadhia samaki ambako nako, alikuta mradi huo, umechelewa kukamilika na kupitisha miaka miwili ya zaidi ya muda uliopangwa kwenye mkataba.
"Hili ni tatizo kubwa katika maeneoyote niliyopita kwenye ziara yangu, nimekumbana na adha hii ya miradi kusimama, kuchelewa na mingine kutelekezwa kwa sababu ya kuchelewa kwa fedha, na hata zikija ni kidogo hazitoshi," alisema.
Aliitaka Serikali kuanza kuchukua hatua za haraka za kurekebisha kasoro hiyo, kwa kuhakikisha fedhaza miradi zinafika maeneo husika kwa wakati muafaka lakini pia kuhakikisha watendaji wasiowajibika wanachukuliwa hatua ikiwemo kufukuzwa.
Awali wakati Kinana akitembelea mradi huo, Mbunge wa Mpanda Vijijini, Moshi Kakoso, alimtaarifu kiongozi huyo, kuwa mkandarasi aliyepewa mradi huo wa bandari ambaye ni Modispan Enterprises, hana uwezo wala utaalamu wa kuukamilisha na jinsi ulivyo ni kama umetelekezwa.
Alisema akiwa kama mbunge aliwasiliana na Serikali kupitia Naibu Waziri wa zamani wa Uchukuzi, Athuman Mfutakamba na kumueleza hali halisi na baadae aliwasiliana na Naibu waziri wa sasa wa wizara hiyo, Dk Charles Tizeba na Waziri wa Uchukuzi Dk Harrison Mwakyembe ambao walimuahidi kushughulikia suala hilo.
Kwa upande wake Diwani wa kata hiyo ya Karema, Michael Kapata, alimuomba Kinana, aingilie kati suala hilo la ujenzi wa bandari kwa kuwa muda mrefu limekuwa likisababisha CCM ichukiwe na wananchi, kwa kuwa mradi huo haueleweki.