RIPOTI YAANIKA MAUAJI YA VYOMBO VYA DOLA

Matukio ya vyombo vya dola kutumia nguvu kupita kiasiyamezidi kuongezeka nchini na kwamujibu wa Ripoti ya Haki za Binadamu ya mwaka 2013 ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), watu 34 waliuawa na watumishi wa vyombo hivyo katika nyakati tofauti.

Ripoti hiyo iliyozinduliwa jana inaonyesha kuwa mauaji hayo yalitekelezwa na baadhi ya askari wa Jeshi la Polisi, Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) na sungusungu. Vyombo vingine vilivyotajwa katika matukio hayo ni polisi jamii na askari wa Wanyamapori. Pamoja na matukio hayo, pia askari wanane waliuawa na raia katika vurugu mbalimbali zilizohusisha pia kuvamiwa kwa vituo vinne vya polisi.


Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk Hellen Kijo-Bisimba alisema matukio hayo yameongezeka kutokana na vyombo husika kutowachukulia hatua maofisa wake baada ya kutekeleza mauaji.

Hata hivyo, Msemaji wa JWTZ, Luteni Kanali Erick Komba alisema jana kuwa baadhi ya askari wa jeshi hilo waliobainika kutekeleza vitendo hivyo walichukuliwa hatua kwa mujibu wa taratibu. Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Isaya Mungulu alisema watatumia ripoti hiyo kujirekebisha zaidi katika utekelezaji wa shughuli mbalimbaliza polisi.


*Maeneo ya mauaji

Dk Bisimba alisema sehemu kubwaya mauaji hayo yalitokea katika matukio baina ya askari na wananchi pia kupitia operesheni zilizotekelezwa na Serikali hususan Operesheni Tokomeza.

"Mambo makubwa matatu ndiyo yalikuwa na uvunjifu mkubwa wa haki za binadamu; Operesheni Tokomeza na Kimbunga pamoja na vurugu za gesi mkoani Mtwara," alisema.

Alisema uvunjifu huo wa amani pia ulitokana na matamko ya viongozi wa Serikali ikiwemo kauli ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda bungeni Agosti mwaka jana, kwamba wananchi wanaovunja amani wapigwe tu na vyombo vya dola.

Alisema mwaka 2013 kulikuwa na matukio ya kutisha ya mauaji kwa mfano, watu kujichukulia sheria mkononi na kuua wengine. Watu 1,669 waliuawa, ikiwa ni ongezeko la vifo 435 kutoka 1,234 mwaka 2012.


"Pia tulishuhudia aina mpya ya mauaji kama vile kumzika mtu akiwa hai kwa imani potofu za kishirikina, kuwapiga mawe na kuwachoma moto watuhumiwa... nivitendo vya kutisha katika utoaji waadhabu ambavyo vinavunja haki za binadamu. Pia kumekuwa na ugumu kwa upande wa polisi na waendesha mashtaka kufanya uchunguzi wa kina na kuwashtaki waliotekeleza vitendo hivyo."


Ripoti hiyo ya kumi na moja tangu zilipoanza kutolewa mwaka 2002, pia imebainisha kuongezeka kwa vitendo vya kuwaua watu kutokana na imani za kishirikina. Watu 765 waliuawa mwaka jana ikilinganishwa na 630 mwaka 2012.

"Kati ya hao waliouawa wanawake walikuwa 505 na wanaume 260," iliongeza ripoti hiyo ikisema mikoa iliyokumbwa zaidi na matukio hayo ni Geita, Mbeya, Shinyanga, Iringa, Tabora na Mwanza.


*JWTZ, Polisi wafafanua

Luteni Kanali Komba alisema: "Ni kweli kumekuwa na baadhi ya wanajeshi wachache kwa kipindi kilichopita, waliofanya vitendo vya uvunjifu wa amani wakiwa katika shughuli za kijamii—nje ya utekelezaji wa majukumu ya kijeshi."

Alisema waliopatikana na makosa hayo walifungwa na wengine kufukuzwa kazi na kwamba katika baadhi ya matukio hayo, wananchi wachache walikuwa chanzo na kusababisha uvunjifu wa sheria.

Alisema JWTZ ni jeshi la wananchi na litaendelea kuenzi dhana hiyo na lina taratibu na sheria mbalimbali za kumwongoza mwanajeshi... "Nidhamu ni suala la msingi kwa mwanajeshi kutokana na dhamana aliyokuwa nayo."

Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali wa Polisi, Ernest Mangu alisema katika taarifa iliyosomwa na DCI Mungulu kuwa matukio hayo ya uvunjifu wa amani hayawezi kuvumiliwa. Aliwataka wadau kushirikiana kuyatokomeza.

"Kufanya vurugu na kuwashambulia raia wengine wakati vyombo vya usalama vipo ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu. Hivyo tukiwa na jamii isiyotii na kuheshimu sheria zilizopo ni hatari kwa amani na utulivu wa nchi yetu," alisema Mangu na kuomba kila mmoja kutimiza wajibu wake ili kulinda haki za binadamu.


Moja wa watafiti walioandaa ripoti hiyo, Pasience Mlowe alisema walikusanya taarifa kutoka katika wilaya 131 kupitia wawakilishi wao na pia kufanya mahojiano ya moja kwa moja katika wilaya 28.