WEZI KUKATWA MIKONO NA WAZINIFU KUPIGWA MAWE

Serikali ya Brunei iliyo Kusini Mashariki mwa Bara Asia, itaanza kutumia sheria kali za kiisilamu.

Kiongozi wa nchi hiyo ya kiisilamu ambayo ni jirani na Malaysia ametangaza kuwa sheria hiyo itaanza kutumika kuanzia wiki hii.


Adhabu zilizo chini ya sheria za kiisilamu ni pamoja na kuwakata wezi mikono na kuwapiga mawe hadi kufa watu waliopatikana na hatia ya kushiriki Zinaa.

Sheria hii itatekelzwa katika awamu tatu katika kipindi cha miaka mitatu.

Umoja wa Mataifa tayari umeelezea wasiwasi wake kuhusu sheria hiyo.


Taifa la Brunei tayari linafuata sheria kali za kiisilamu kuliko hata nchi jirani kama Malaysia na Indonesia pamoja na kuharamisha uuzaji na utumiaji wa pombe.


Nchi hiyo ndogo ilio katika kisiwa cha Borneo, inatawaliwa na Sultan Hassanal Bolkiah na imepata utajiri wake kutokana na kuuza nje mafuta na gesi yake.

Takriban nusu ya waisilamu wanaoishi katika nchi hiyo ni raia wa Malaysia.


Sultani alinukuliwa akitangaza hatua ya kwanza ya kuanza kutumiwa kwa sheria hiyo akimshukuru Mungu na kuwatahadharisha wananchi kuhusu kuanza kutumika kwa sheria hiyo.


Sheria yenyewe itaanza kutumika katika kipindi cha miaka mitatu huku hukumu ya makosa ya kwanza ikiwa kifungo cha jela pamoja na kutozwa faini.


Katika awamu ya pili ndipo wahalifu wataanza kukatwa mikono kwa watakaopatikana na hatia ya wizi , huku awamu ya tatu ikihusu kupigwa mawe wazinifu na wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja.


Sultani anayetawala kisiwa hicho ni mmoja wa matajiri wakubwa duniani na tayari amewaonya watu kukoma kushambulia mipango yake kupitia mitandao ya kijamii.

Mfumo wa sheria katika mahakama nchini humo ni sawa na ule wa Uingereza.


Umoja wa Mataifa uliitaka serikali kuchelewesha mageuzi hayo ili kuhakikisha kuwa sheria hiyo inaambatana na sheria za kimataifa kuhusu haki za binadamu.