Timu hiyo ya wataalamu itakayoongozwa na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI),Issaya Mngulu, itaongeza nguvu ili kuhakikisha kwamba wote wanaojihusisha na vitendo hivyo wanakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria haraka.
Jeshi la Polisi nchini limewaomba wananchi, wenye taarifa za wahalifu hao, kutoa taarifa hizo kupitia namba za simu 0715 009930 na 0754 785557 au katika kituo chochote cha Polisi.
Habari kutoka mtandao wa kijamii wa http://www.jambotanzania.com, unaohusisha mabloga wanaodhaminiwa na Mfuko wa Kusaidia Vyombo vya Habari (TMF), zimesema kwamba mauaji hayo, yanafanywa kwa sababu za kishirikina.
"Mauaji ya wanawake mkoani Marahususani wilayani Butiama, hufanywa kwa sababu za kijinga na zisizo na ukweli za haja ya kupata samaki wengi kwa kutumia viungo vya mwanamke, ambavyo hudaiwa kuvuta samaki," umeandika mtandao huo kupitia mwandishi wake, homari Binda.
Mtandao huo ambao umedai kufanya utafiti wa kina, umesema wauaji ni wale wanaojishughulisha na uvuvi, wakiwa na imani kuwa wanapomuua mwanamke na kuchukua baadhi ya vitu kwenye mwili wake kama sehemu ya siri na nywele za ukeni, hupata samaki wengi wanapoenda kuvua.
Serikali na viongozi wa dini wamefanya jitihada kubwa, kukomesha mauaji hayo. Kwa mujibu wa taarifa za kipolisi, zilizonukuliwa na mtandao huo ni kuwa katika kipindi cha miezi mitatu, wanawake zaidi ya 15 wameuawa.
Miongoni mwa waliouawa ni Catherine Mandela (21) kutoka kijiji cha Kigera Etuma Tarafa ya Kusenyi wilayani Butiama. Taarifa za awali zilizoonesha kwamba mwanamke huyo, kauawa kwa imani za kishirikina.
"Huyu ni mwanamke wa pili katika kipindi cha mwezi mmoja kuuawa katika eneo letu katika mazingira ambayo naweza kusema ni imani za kishirikina na mahitaji ya utajiri wa haraka kwa wanadamu wasiomuogopa Mungu," alisema Maiga Maingu wa Kijiji cha Kigera Etuma.
Alisema imani za kishirikina ndio chanzo kikubwa cha mauaji hayo.
Alidai kuwa wanaotekeleza mauaji hayo ni wale wanaojishughulisha na uvuvi kwenye kambi za uvuvi, wakiamini wanawake wana mvuto wa kuvuta samaki kwenye mitego.
Maingu ambaye ni mvuvi mstaafu, alisema kwa sasa imani hiyo imeshika kasi na wanawake wengi wamekuwa wakiuawa, kutokana na imani hiyo potofu.
Masatu Mfungo wa Kijiji cha Esiri Kata ya Kigera Etuma, alisema kuibuka kwa mauaji hayo ya wanawake, kumewafanya wanawake kwenye Kijiji hicho, kuogopa kwenda kulima shambani.
Mwanamke mwingine aliyeuawa niwa Kijiji cha Nyegina Kata ya Nyegina wilayani Butiama, Mkaguru Magee, ambaye aliuawa shambani kwake na kisha kufukiwa shambani.
Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, John Tupa alipambana vikali kuhakikisha mauaji dhidi ya wanawake Butiama yanakomeshwa. Kabla hajafariki, aliagiza kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa kujitahidi kukomesha mauaji ya wanawake yanayoendelea Butiama.