Tukio hilo ambalo ni mfululizo wa vijembe, baina ya wajumbe wa CCM na upinzani, kuhusu hoja ya serikali tatu au mbili, lilisababisha viwanja vyote vya bunge jana mchana, kutawaliwa na kelele za kushangilia na kuzomeana.
Akitoa ufafanuzi wa kamati namba 11, Duni alisema siyo serikali tatu ni ufumbuzi wa malalamiko ya Muungano, ambayo yanaifanya Zanzibar kuendelea kubanwa na kushindwa kuwapatia maendeleo wananchi wake.
Alisema serikali iliyopo madarani kwa miaka 50 sasa, imeshindwa kutumia rasilimali zilizopo Zanzibar na kuifanya iwe kutovu cha utalii katika ukanda wa Afrika Mashariki na kati badala yake inazuia kila jambo jema la maendeleo.
"Kama mngekuwa na dhamira ya dhati na Zanzibar, leo Zanzibar ingekuwa kama Hong Kong ya Afrika lakini hakuna, Zanzibar imefungwa mikono na miguu hata kutembea haiwezi," alisema.
Alisema hoja kuwa katika muundo wa serikali tatu, ukianza Zanzibar haiwezi kuchangia Muungano siyo ukweli kwani, uchumi wa wananchi wa Zanzibar hauna tofauti na uchumi wa Watanganyika kwa mtu mmoja moja. Akizungumzia takwimu za tume ya mabadiliko alisema zipo sahihi kuwa waliotaka Muungano wa Serikali tatu ni wengilakini kinachofanywa na wanaotaka serikali mbili ni kupotosha ukweli.
Haji alitolea mfano katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, kuwa walioandikishwa kupiga kura walikuwa ni watu 20 milioni, waliopiga kura ni watu milioni nanena ambao walimchagua Rais Jakaya Kikwete ni watu milioni sita hivyo kwa hoja ya wanaCCM kuhusu Rasimu ina maana watu 14 milioni hawamtaki Rais Kikwete.
Akizungumzia gharama za Muungano, alisema fedha nyingi zaidi ya asilimia 70 za Muungano, zinatumika katika kuendesha Serikali ya Tanganyika jambo ambalo siyo sahihi.
Huku akitoa takwimu mbalimbali, alisema kwa maana hiyo uchangiaji wa Muungano kamwe hauwezi kuwa sawa kwa pande zote. "Katika jambo moja tu la askari polisi, tafitiza kimataifa zinaonesha kuwa askari mmoja anafaa kulinda watu 400, kwa Zanzibar yenye watu 1.3 milioni inahitaji askari 3,000 tu, lakini Tanganyika yenye watu zaidi ya 40 milioni inahitaji zaidi ya askari 120,000 hivyo uchangiaji wa Muungano hauwezi kuwa sawa," alisema.
Haji pia alieleza kuwa, hati za Muungano ambazo waliowengi wanasema zinamsingi wa serikali mbili, siyo kweli bali hati hizo zinatambua serikali tatu, ikiwapo ya Tanganyika.
Hata hivyo, alisema msingi wa serikali mbili ni mkakati wa CCM ambao ulianza tangu enzi za TANU mwaka 1977, kutaka kuwa na serikali moja na hivyo, kuifanya Zanzibar kuwa siyo nchi.