KITUO CHA MABASI CHALIPULIWA NIGERIA

Milipuko miwili imetokea katika kituo cha mabasi katika vitongoji vya mji mkuu wa Nigeria, Abuja, na kuna taarifa ya watu wengi kujeruhiwa kwa mujibu wa watu walioshuhudia tukio hilo.

Mwandishi wa BBC, nchini Nigeria, Haruna Tangaza anasema milipuko hiyo ilitokea wakati abiria wakiwa katika harakati za kupanda mabasi na teksi wakienda maofisini katikati ya mji wa Abuja.

Shirika la habari la Uingereza, Reuters, limewakariri watu walioshuhudia tukio hilo wakisema mabasi mawili yaliyokuwa yamejaa abiria yalilipuliwa.

Mmoja wa mashuhuda wa shambulio hilo, Badamsi Nyanya ameiambia BBC kuwa ameona miili 40 ikiondolewa.

"Asubuhi hii kulikuwa na mlipukokatika eneo la maegesho ya magari ya Nyanya Motor Park," anasema Manzo Ezekiel wa Wakala wa Usimamizi wa Taifa wa Majanga.

Vikosi vya uokoaji tayari vipo katika eneo la tukio.

Shuhuda mwingine Bi Mimi Daniels, ambaye anafanya kazi mjini Abuja, anasema: "nilikuwa nasubiri basi niliposikia mlipuko mkubwa halafu nikaona moshi," ameiambia Reuters.

"Watu walikuwa wakikimbia ovyo kutokana na taharuki."