WALIOFARIKI KATIKA FERI WAFIKIA 113

Idadi ya watu waliofariki kutokana na ajali ya feri iliyozama wiki jana nchini Korea Kusini imefika 113.


Wapiga mbizi walipata miili zaidi hii leo ndani ya Feri hiyo. Wamekuwa wakijaribu kufikia sehemu ya mkahawa wa feri hiyo ambako wanatarajia kupata miili zaidi.

Watu 190 bado hawajapatikana , wengi wao wakiwa ni wanafunzi wa shule ya sekondari iliyo karibu na mji mkuu Seol.

Wahudumu wa feri hiyo bado wanazuiliwa kwa kusababisha ajali hiyo hasa baada ya Rais wa taifa hilo kusema hapo jana kuwa kitendo chao kinatosha kuwa mauaji.

Maafisa wanasema wataanza juhudi za kuiondoa Feri hiyo kutoka majini Siku ya Alhamisi baada ya mashauriano na ndugu wa waathiriwa wa ajali hiyo.


Feri hiyo ilizama katika muda wa saa mbili wiki jana na haijulikani kilichosababisha ajali hiyo.

Wafanyakazi wa feri hiyo wanalaumiwa kwa kukosa kuwaokoa abiria wengi waliokuwa wameabiri feri hiyo.

Watano kati yao tayari wamefunguliwa mashitaka ya kuzembea katika kazi ya kuwaokoa waathirwa.

Wakati meli hiyo ilipokuwa inazama, abiria wanadai kuwa waliambiwa kusalia ndani ya ferry na kujifungia katika baadhi ya vyumba huku kukizuka hali ya wasiwasi ikiwa abiria waondoke kwenye Feri.

Inaarifiwa kilio cha kwanza cha kutaka msaada kilitoka kwa kijana mmoja akiwa na uoga na kisha kufuatiwa na simu nyingine kutoka kwa wanafunzi 20 wakitaka kusaidiwa.


Takriban abiria 174 waliokolewa kutoka kwa feri hiyo iliyokuwa imewabeba watu 476 ikiwemo wanafunzi 339 pamoja na walimu waliokuwa wanafanya ziara ya kimasomo.