Hasira yao inatokana na madai kwamba maoni ya wananchi yaliyowasilishwa na Tume ya Marekebisho ya Katiba Mpya yamekuwa yakipuuzwa.
Wajumbe wa bunge hilo ambao ni kutoka upande wa upinzani chini ya umoja unaojulikana kama UKAWA, yaani Umoja wa Katiba ya Wananchi, wameamua kutoka nje kupinga kile wanachosema ni kupuuzwa kwa makusudi maoni ya wananchi wanaotaka muungano wa muundo wa serikali tatu kama yalivyopendekezwa katika rasimu ya katiba hiyo.
Kilio cha mwananchi
Akichangia katika kikao cha bunge hilo Jumatano jioni, mmoja wa wajumbe Profesa Ibrahim Lipumba amelalamikia kauli za ubaguzi zinazotolewa na baadhi ya wajumbe, hususan wanaotaka muundo wa muungano wa serikali mbili, alieleza sababu za kutaka serikali tatu kuwa zitasaidia kutatua matatizo yaliyopo katika muundo wa sasa.
Hata hivyo hakusita kupinga kile anachokiita kauli za ubaguzi kutoka kwa wajumbe wanaopinga mawazo ya wachache bungeni humoi.
"Hatuwezi kuwa kama kundi la wapiganaji linalohamamisha ubaguzi ndani ya Tanzania, hili hatulikubali, hatulikubali, hatulikubali, watu wote tunaotaka katiba ya wananchi tunawaachia muendelee na kikao chao. Ahsanteni sana".
Mara baada ya kusema hivyo, wajumbe waliounga mkono kauli yake waliinuka na kutoka nje.
Hata hivyo, kikao cha bunge hilo kiliendelea baada ya makamu mwenyekiti wa bunge hilo kusema idadi ya wajumbe waliobaki walitosha kuendelea na kikao hicho.
Muundo wa serikali
Wanaounga mkono muundo wa serikali tatu, wanasema muundo wa sasa wa serikali mbili umeshindwa kutatua masuala yenye mgogoro katika muungano, maarufu kama kero za muungano, hivyo kudhoofisha muungano huo.
Hata hivyo wajumbe wanaounga mkono serikali mbili, yaani serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wanasema muundo wa serikali tatu ni kuvunja muungano wa Tanganyika na Zanzibar na pia itakuwa gharama kuiendesha serikali ya tatu.Bunge hilo lenye zaidi ya wajumbe mia sita linaundwa na wabunge wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Baraza la wawakilishi Zanzibar na wajumbe 201 walioteuliwa narais wa Tanzania kutoka makundi mbalimbali ya kijamii.
Wajumbe 191 kutoka upinzani walitoka nje ya bunge kupinga mwenendo wabunge hilo katika kujadili rasimu ya katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.