ZITTO: SERIKALI 3 HAZITA VUNJA MUUNGANO

Mjumbe wa Bunge la Katiba, Zitto Kabwe amesema kuandikwa kwa Katiba isiyokubaliwa na pande zote kutasababisha gharama kubwa kuliko zile zinazotajwa za serikali tatu.

Akichangia hoja kwenye Bunge hilo jana, Zitto alisema kuna kila sababu ya kukaa na kukubaliana ili kupata Katiba itakayokubalika pande zote.

"Muundo wa Muungano una hatari ya kuvunjika iwapo hakuna matakwa ya dhati ya watu kuungana... Maneno ya kusema Serikali tatu zitavunja Muungano ni ya siasa na hayana msingi wa kisayansi. Urusi ilivunjika sababu haikuwa na demokrasia na siyo sababu ya idadi ya Serikali,"alisema.

Zitto ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali(PAC), alisema hofu ya gharama inayotajwa katika uendeshaji wa muundo wa serikali tatu haina msingi wowote kwa kuwa hakuna ushahidi wa kitaalamu unaothibitisha gharama hizo.

"Nimesikia watu wanasema eti tutalazimika kujenga ikulu mpya, nani kasema lazima tuwe na marais watatu? Tunaweza kuwa na rais mmoja kwenye nchi na wakuu wa nchi washirika wawili… Ni jambo la makubaliano tu," alisema.

Alisema bajeti ya mwaka huu ni Sh18 trilioni, kati ya hizo Sh5.3 trilioni ndizo zinazohudumia wizara za Muungano, lakini serikali ina uwezo wa kukusanya kodi zaidi ya Sh10 trilioni pamoja na mapato mengine."
Kuna jumla ya Sh2.3 trilioni hatuzikusanyi kila mwaka kutoka kwenye kampuni kubwa, kwa uwezo wetu wapato la ndani asilimia 17 tunao uwezo wa kuendesha serikali ya muundo wa idadi yoyote.

"Hofu ya Serikali ya Muungano kutokuwa na fedha ni sababu halisi, ni kweli kwamba ushuru wa bidhaa pekee yake hauwezi kutuendeshea serikali. Sasa nini kazi yetu, tunaingia hapa ili kuboresha hayo maeneo, kama hatuwezi tumekuja kufanya nini hapa?" alihoji.