DK. BILALI MKUMZIKA GURUMO LEO

Makamu wa Rais Dk.Gharib Bilal anatarajiwa kuongoza msafara wa mazishi ya mwanamuziki nguli Muhidin Maalim Gurumo yatakayofanyika leo katika Kijiji cha Masaki Wilaya ya Kisarawe Pwani.

Dk. Bilal ataambatana na viongozi wengine wa Serikali na wasanii mbalimbali katika mazishi ya nguli huyo aliyefariki Aprili 14 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) alikokuwa amelazwa kwa matibabu ya ugonjwa wa moyo uliomsumbua kwa muda mrefu.

Akizungumza jana nyumbani kwa marehemu Mabibo External, msemaji wa familia Yahya Mikole alisema marehemu anatarajiwa kuzikwa leo mchana, nyumbani kwao Masaki kabla ya kusomewa dua asubuhi ya saa tatu nyumbani kwake jijini.

Mke wa mwanamuziki huyo Pili Kitwana akizungumza kwa uchungu, alisema kuwa haamini kama mtu aliyeishi naye kwa miaka zaidi ya 40, amemtoka.

"Ninachoweza kusema ni kumshukuru Mungu kwa kuwa kazi yake haina makosa, namuombea apumzike kwa amani."

Wakati huohuo;Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete amemtuma salamu za rambirambi kwa familia ya mwanamuziki huyo.

"Nimesikitishwa na kuhuzunishwa na taarifa za kifo cha Muhidini Maalim Gurumo ambaye alikuwa mmoja wa wasanii wa muziki wa dansi nchini, waliolitumikia Taifa hili kwa bidii tangu miaka ya sitini kupitia sanaa ya muziki katika bendi mbalimbali za muziki wa dansi, kuanzia Bendi ya NUTA Jazz, Mlimani Park Orchestra, Orchestra Safari Sound (OSS) na Msondo Ngoma ambayo ameitumikia hadi alipostaafu mwaka 2013", alisema Rais Kikwete katika salamu zake.