KAFULILA ASISIMUA BUNGE

Mjumbe wa Bunge la Katiba, David Kafulila jana aligeuka shujaa bungeni na kubebwa juujuu na wajumbe wenzake kutoka kundi la walio wachache baada ya 'kusambaratisha' hoja za wajumbe wanaopinga Serikali tatu.

Kafulila ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), alifanya hivyo alipokuwa akifafanuahoja kutoka kundi la walio wachache katika Kamati Namba Tano.

Miongoni mwa hoja ambazo alizijibu na kushangiliwa na wajumbe, ni juu ya gharama za Serikali tatu, kuwa zitavunja Muungano, kwamba Serikali ya Muungano itakosa mapato, hoja ya kumuenzi Mwalimu Julius Nyerere na uhalali wa takwimu za Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Alisema hoja kuwa Serikali tatu ni kuvunja Muungano si za kweli, akisema ni propaganda zilezile ambazo CCM ilizitumia mwaka 1992 kutembea nchi nzima kupingamfumo wa vyama vingi.

"Wakati ule CCM ilitembea nchi nzima huku wakionyesha video kuwa vyama vya upinzani vitaleta vita, lakini leo miaka 20 baada ya kukubali mfumo wa vyama vingi hakuna vita vilivyoletwa na upinzani," alisema Kafulila. Alisema haiwezekani tume zote ambazo zinaundwa na Serikali zipendekeze serikali tatu na kila wakati serikali iliyopo madarakani ikatae.

"Hoja ya serikali tatu siyo hoja ya Warioba, tume zote zilizowahi kuchunguza muundo ya Muungano zote zilipendekeza serikali tatu," alisema na kuongeza: "Ofisi ya Rais ilipendekeza serikali tatu, ofisi ya Waziri Mkuu ilipendekeza serikali tatu, inatuwia vigumu ndani ya muda mfupi, vyombo hivi vibadilike na kutaka serikali mbili." Alisema wanaotaka serikali tatu wanataka kwa namna ambayo inaimarisha Muungano, tofauti na maoni ya walio wengi kuwa serikali ya Muungano itakuwa legelege kwa kuwa itakosa nguvu za kiuchumi.

"Ni kweli inawezekana vyanzo vya mapato vilivyopendekezwa havitoshi kuendesha Bunge, lakini ndiyo sababu tupo hapa, haiwezekani ripoti ya Tume iwe imekamilika pande zote," alisema na kuongeza:

"Wamependekeza badala ya kutegemea vyanzo vya washirika, tumependekeza kodi ya bandari ambayo ni karibu Sh 3.6 trilioni inaweza kuwa ni kodi ya Serikali ya Muungano. Kodi hiyo pekee inatosha kuendesha wizara zote ambazo gharama yake si zaidi ya Sh 3 trilioni."

"Kuna hoja hapa, haiwezekani kuwa fedha za bandari zote ziwe zinachangia Muungano kwani ni fedha za Tanganyika, lakini Muungano wowote ni lazima kukubali nchi kubwa kuchangia zaidi."

Kafulila ambaye hata baada ya kumaliza muda wake wajumbe walipiga kelele wakitaka aendelee, alisema kwa Serikali ya Muungano kupata mapato hayo tu, itakuwa haina haja ya kusubiri fedha za nchiwashirika na pia itakuwa na uwezo wa kuchangia fedha kwa nchi washirika.

"Haiwezekani Watanganyika wakubali kubeba gharama kubwa yaserikali mbili badala ya gharama ndogo za serikali tatu na hii ndiyo inawapa hofu Wazanzibari kudhani kuna kitu kinachofichwa," alisema. Kuhusu hoja ya kutumia maneno ya Nyerere kupinga Muungano wa serikali tatu, alisema Mwalimu hakuwa nabii, alitazama mambo kwa wakati ule na alikuwa akibadilika kutokana na wakati.

Alisema mwaka 1965, Mwalimu Nyerere alifuta vyama vingi... "Angekufa mwaka huo, tungebaki kuwa alikataa vyama vingi, lakini Nyerere huyu mwaka 1992 alikubali vyama vingi na hiyo inaonyesha kuwa kila jambo lina wakati wake na kwa sasa hakuna namna na kupinga serikali tatu. Hivi sasa tunapata ugumu wa lazima kutokana na misimamo ya vyama, lakini katika jambo hili la serikali mbili na tatu na wengi wameamua."

Alisema suala hilo likiachwa kama lilivyo waliopo madarakani sasa wataendelea kulifunika lakini itakuja kuwa hasara kwa nchi: "Leo mna nafasi ya kutengeneza serikali tatu kiuhalisia zaidi kuliko baadaye, mtakosa nafasi hii, huko baadaye haiwezekani kuwa na wingi huu, leo mnaweza kuamua serikali bora zaidi, huu ni wasia tu," alisema huku akishangiliwa.

Akizungumzia uwiano, alisema mataifa yote duniani yanapoungana huwa hayana uwiano ulio sawa.

Alisema Jimbo la California peke yake nchini Marekani linachangia zaidi ya asilimia 20 ya mapato yote.

Baada ya kutoka nje ya Ukumbi wa Bunge, Kafulila ambaye alichambua kwa kina takwimu za Tume ya Warioba alipokewa kwa shangwe na wajumbe wa kundi la Ukawa, wakimsifia kwa kuzungumza kishujaa.