Wanafunzi 15 Washikiriwa na Polisi

Wanafunzi 15, wa Shule ya Sekondari ya
Jumuiya ya Wazazi ya Lupata wilayani Rungwe
mkoani Mbeya , wanashikiliwa polisi kwa
tuhuma za kuchoma moto bweni la wanafunzi
wa kiume na kusababisha uharibifu wa mali
mbalimbali.

Aizungumzia tukio hilo , Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Mbeya, Diwani Athuman, alisema tukio
hilo lilitokea juzi saa 2:00 usiku shuleni hapo  na
kwamba wanafunzi hao walifikia hatua hiyo ya
kuchoma moto bweni hilo, wakipinga
kusimamishwa masomo kwa wanafunzi wenzao
watatu kwa utovu wa nidhamu.

Aliwataja wanafunzi waliosimamishwa masomo
kwa utovu wa nidhamu kuwa ni Joseph Robert
(18), anayesoma kidato cha nne na Mwita Chacha
(17) na anayesoma kidato cha tatu, wote wakazi
wa Kitunda jijini Dar es Salaam na Mwingine ni
Daniel David (18), anayesoma kidato cha tatu
ambaye ni mkazi wa Ipinda wilayani Kyela.

Alisema kuwa wanafunzi hao watatu
waliwahamasisha wenzao kuwaunga mkono
kupinga adhabu hiyo kwa kufanya vurugu na
kwamba bweni lililochomwa moto walikuwa
wanaishi wanafunzi 50, ambao hawakuwa tayari
kuunga mkono uvunjifu huo wa amani.