Mwenyekiti wa baraza la kitaifa la
Congress nchini Libya amejiuzulu
kufuatia kupitishwa kwa sheria mpya
inayoharamisha yeyote aliyefanya kazi
katika serikali ya hayati Muamar
Gaddafi kushikilia wadhifa wowote
katika serikali ya sasa.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya
habari, Muhammad al-Magarief
alisema kuwa bunge ilipitisha sheria
inayowatenga watu waliofanya kazi
katika serikali ya Gaddafi, na kuwa kila
mtu anapaswa kuitii sheria hiyo.
Aidha sheria hiyo, imekosolewa sana
kwa kuwa na nguvu sana.
Kanali Gaddafi aliondolewa
mamlakani mwezi Agosti mwaka
2011.
"najiuzulu na ninafanya hivyo kwa
roho safi nikiwa najivunia kwa kufanya
hivyo," alisema bwana Magarief,
alipokamilisha hotuba yake ya dakika
40, kwa baraza la Congress.
Hata hivyo haijulikani kwa sasa ikiwa
wanachama wa Congress,
wanahitajika kupiga kura kuhusu ikiwa
watalikubali au kulikataa ombi la
bwana al-Magarief kujiuzulu.
Hata hivyo, kufuatia taarifa yake,
msemaji wa Congress, Omar
Hmeidan, alisema kuwa baraza la
Congress litahitajika kumteua
mwenyekiti mwengine.
Chini ya sheria mpya, mabalozi
waliofanya kazi chini ya utawala wa
Gaddafi hawawezi kuendelea
kushikilia nyadhifa zao.
Kulikuwa na mjadala mkali kuhusu
mabadiliko yanayofanyiwa sheria
hiyo, kuruhusu baadhi ya maafisa
kushikilia nyadhifa hiyo , lakini hilo
bado halijafanyika.
Dr Magarief alihudumu kama balozi
nchini India, kwa miaka miwili, katika
miaka ya themanini kabla ya
kuondoka katika serikali ya Gaddafi.
Aliishi uhamishoni kwa miaka 31 kama
kiongozi wa vuguvugu la ukombozi
wa Libya.