Ratiba Ya Kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika Yapangwa

Michuano ya kufuzu kwa fainali ya
kombe la mataifa bingwa barani
Afrika ACN, mwaka wa 2015,
itachezwa kwa muda wa miezi mitatu
pekee mwaka Ujao.
Tangazo hilo limetolewa na shirikisho
la mchezo wa soka barani Afrika CAF.

Uamuzi huo sasa unamaanisha mechi
mia moja na arubaini na nne,
zinazojumuisha timu 48, katika
makundi 12 ya timu nne kila mmoja
itachezwa kati ya Septemba na
Novemba mwaka ujao.
Ratiba hiyo mpya, imepangwa ili
kuwiana na ratiba ya mechi za
kimataifa ya shirikisho la mchezo huo
duniani FIFA.

Vile vile mashindano hayo
hayatakuwa na nafasi mwaka wa
2014, kabla ya fainali za kombe la
dunia itakayoandliwa nchini Brazil.

Hii ni mara ya kwanza kwa fainali hizo,
kuandaliwa nje ya mwaka ambao
fainali za kombe la dunia kufanyika,
tangu ilipoamuliwa kuwa mashindano
hayo yafanyike mwaka mmoja kabla
na baada ya fainali za kombe la dunia.

Na kutokana na matatizo ya usafiri
barani Afrika, ratiba hiyo mpya
huenda ikakumbwa na matatizo hasa
kutoka mashariki hadi magharibi mwa
Afrika.

Matatizo ya fedha

Timu itacheza mechi moja mwishoni
mwa wiki na kupumzika kwa siku mbili
kabla ya kucheza mechi nyingine
kuambatana na ratiba ya FIFA.

Wachezaji wanaoshiriki ligi za kulipwa
ni sharti waruhusiwe na vilabu vyao
kuaklisha mataifa yao katika mechi
hizo.

Mechi hizo zimepangiwa kuchezwa
kati ya tarehe Moja hadi Tisa
Septemba, kisha tarehe Sita hadi
tarehe Kumi na Nne Oktoba na mechi
za mwisho zitachezwa kuanzia tarehe
Kumi hadi Kumi na Nane Novemba.

Rais wa shirikisho la mchezo wa soka
nchini Namibia, John Muinjo,
anaamini ratiba hiyo mpya itawapa
changamoto nyingi.

Amesema kucheza mechi sita za
kimataifa kwa muda wa miezi mitatu
itakuwa ngumu sana na hatari hata
kwa afya ya wachezaji.

Aidha amesema kutokana na matatizo
wa fedha, wasimamizi wa soka katika
nchi kadhaa huenda wakashindwa
kuwasafirisha wachezaji wao kutoka
nchi moja hadi nyingine kwa muda
mfupi.

Baada ya kukamilika kwa hatua ya
makundi, washindi wa kila kundi
watajumuika na timu zingine tatu
zilizoandikisha matokeo mema zaidi
katika makundi yao kufuzu kwa kwa
hatua ya mwisho ya kufuzu ambayo
itaandliwa nchini Morocco kati ya
mwezi Julai na Agosti mwaka wa 2015.