Lipumba Muongo "Ikulu"

KAULI ya Mwenyekiti wa
Chama cha Wananchi (CUF),
Profesa Ibrahim Lipumba,
kwamba kuna njama za
kumwongezea Rais Jakaya
Kikwete, muda wa kuongoza
nchi, ni uzushi mtupu na ni
upotoshaji usiokuwa na
msingi.

Taarifa ya Kurugenzi ya
Mawasiliano ya Ikulu
iliyotumwa kwa vyombo vya
habari juzi, ilifafanua kwamba
Rais Kikwete hafahamu
kuwepo mipango hiyo, na
kumtaka Profesa Lipumba
aisaidie jamii kusema nani
anafanya mpango huo, ili
ukweli ujulikane.

“Aidha, Mheshimiwa Rais
anawasihi wanasiasa na
Watanzania kwa ujumla,
kuacha tabia za uongo na
uzushi na kuwapotezea muda
Watanzania kufikiria mambo
yasiyokuwepo.

“Ukweli ni kwamba, kama
ambavyo amesema mara
nyingi, ni matarajio ya Rais
Kikwete kuwa mchakato wa
Katiba utakamilika mwaka
2014, na kuwezesha Uchaguzi
Mkuu wa 2015 kufanyika chini
ya Katiba Mpya kama
inavyotarajiwa ,” ilieleza
taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa Ikulu, Rais
Kikwete anatarajia baada ya
uchaguzi wa 2015, atapata
nafasi ya kustaafu mwisho wa
kipindi chake cha uongozi kwa
taifa letu.