WAZIRI wa Ujenzi, Dk John
Magufuli amesema serikali
inaendelea kujenga barabara
kwa kiwango cha lami ifikie
hatua ya watu wasafiri kutoka
Burundi hadi Dar es Salaam
kwa teksi na ikiwezekana kwa
bajaj.
Dk Magufuli alisema hayo jana
bungeni wakati akijibu
maswali bungeni likiwemo la
Mbunge wa Kigoma Kaskazini,
Kabwe Zitto aliyesema Kigoma
imefaidika na barabara lakini
hazina maana kama barabara
za kuiunganisha na Tabora
hazitengenezwi.
“Namshukuru Zitto kwa
kupongeza Serikali ya CCM.
Ni
kitendo cha ushujaa kwa
mbunge wa kambi ya upinzani
kupongeza…barabara (za
Tabora) zimeshawekewa jiwe
la msingi, zitaendelea
kujengwa watu watoke
Burundi hadi Dar es Salaam
kwa teksi na ikiwezekana kwa
bajaj,” alisema Magufuli.
Akielezea kusimama kwa
ujenzi wa barabara za Tabora-
Nzega, Tabora-Urambo na
Kaliua, Waziri Magufuli
alisema miezi miwili iliyopita
kulikuwa na mvua nyingi
ambazo ziliathiri matengenezo
yake. Akizungumzia maeneo
ya barabara yaliyoharibika
baada ya ujenzi, Magufuli
alisema wizara inachukua
hatua.
Mojawapo ni mkandarasi
aliyerudishwa katika eneo la
Sekenke kurudia ujenzi kwa
gharama zake na amepewa
mwaka mmoja wa uangalizi
wa barabara hiyo.
Hata hivyo, Waziri Magufuli
alisema serikali iko katika
mchakato wa kupitia sheria
kudhibiti uzidishaji wa mizigo
kutokana na ukweli kwamba
Tanzania ndiyo inaruhusu tani
nyingi kupitishwa barabarani
ikilinganishwa na nchi
nyingine zikiwemo
zilizoendelea.
Kwa mujibu wa Magufuli,
kiwango cha tani
zinazoruhusiwa nchini ni 56
wakati nchi kama vile
Marekani, kiwango chao ni
tani 40, Uingereza ni 44,
Denmark tani 48; Uganda na
Kenya zinaruhusu tani 54.
Awali katika swali la msingi,
Mbunge wa Viti Maalumu,
Martha Mlata (CCM) alihoji
utekelezaji wa ahadi ya
Serikali kwamba katika
awamu ya nne wananchi
wataweza kusafiri kwa teksi
kutoka Mtwara hadi Bukoba.
Akijibu swali hilo, Naibu
Waziri wa Ujenzi, Gerson
Lwenge alisema lengo hilo
limetekelezwa kwa mafanikio
makubwa hadi kufikia asilimia
99 ya barabara yote kutoka
Mtwara hadi Bukoba.
Alisema barabara yote kuanzia
Mtwara-Dar es Salaam-
Dodoma-Singida-Nzega-Tinde-
Usagara-Geita-Bwanga-
Kyamyorwa hadi Bukoba
yenye urefu wa kilometa
zipatazo 1,989 imejengwa kwa
kiwango cha lami isipokuwa
eneo la urefu wa kilometa 26
katika barabara ya Ndundu-
Somanga litakalokamilika
Desemba mwaka huu.