Polisi Wadakwa na Bangi

Siku chache baada ya Jeshi la Polisi
Kanda Maalumu ya Dar es Salaam
kuwakamata askari 16
wakituhumiwa kujihusisha na
biashara ya magendo, askari
wengine wawili wa jeshi hilo
wamekamatwa mkoani Kilimanjaro
wakiwa na shehena kubwa ya bangi
wakiisafrisha kwenda nchini Kenya.

Askari hao walikamatwa Mei 19
mwaka huu saa nne usiku eneo la
Kilemapofu, Wilaya ya Moshi Vijijini
wakiwa na magunia 18 ya bangi
ambayo walikuwa wameyapakia
kwenye gari la Mkuu wa Kikosi cha
Kutuliza Ghasia (FFU) mkoani
Arusha aina ya Toyota Land Cruiser
lenye namba PT 2025.
Akithibitisha kukamatwa kwa askari
hao, Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Kilimanjaro, Robert Boaz alisema
askari hao walikuwa wakipeleka
bangi hiyo Wilaya ya Rombo kwa
mfanyabiashra mmoja ambaye
hakutaka kumtaja jina lake.

Kamanda Boaz aliwataja askari
waliokamatwa na wanashikiliwa
kwenye kituo kikuu cha polisi katika
mji mdogo wa Himo kuwa ni F.1734
Koplo Edward (dereva) wa kikosi
cha kutuliza ghasia (FFU) mkoani
Arusha na G.2434 Konstebo George
wa kituo cha polisi Ngarenanyuki
Wilaya ya Arumeru.
Alibainisha kuwa kukamatwa kwa
askari hao kunatokana na
operesheni ya kukabiliana na dawa
za kulevya inayofanywa na polisi
katika mikoa ya Arusha na
Kilimanjaro.

Alisema operesheni hiyo imefanyika
kikamilifu katika Mkoa wa Arusha
uliokuwa ukitumika kupitishia
bidhaa hiyo, na sasa wahusika
wameamua kuutumia Mkoa wa
Kilimanjaro.

“Baada ya kuwahoji askari wale,
walidai kuwa walikodishwa na
mfanyabiashara huyo kuipeleka
bangi hiyo wilayani Rombo tayari
kwa kusafirishwa kwenda nchini
Kenya ambako inaaminika kuna
soko kubwa,” alisema.
Kamanda Boaz alisema hivi sasa
polisi wa Kilimanjaro kwa
kushirikiana na wenzao wa Arusha
wanafanya uchunguzi kubaini
mtandao wa askari hao
unaojihusisha na vitendo haramu.

Aliongeza kuwa hatua inayofuata
kwa askari hao ni kufunguliwa
mashtaka ya kijeshi na iwapo
watakutwa na hatia watafukuzwa
kazi kisha watafikishwa katika
mahakama za kiraia.
Kamanda Boaz alibainisha kuwa
kwa kawaida askari wanapotoka
mkoa mmoja kwenda mwingine
hupatiwa kibali maalumu cha
kusafiria (Movement Order).

Alisema kibali hicho husaini kila
mkoa ambao askari husika hupita,
lakini waliokamatwa na bangi
hawakuwa nacho.
Kamanda Boaz alibanisha kuwa kwa
hali ilivyo askari hao waliondoka na
gari la mkuu wa FFU bila kumpa
taarifa wala kupata kibali chake.

Tanzania Daima limedokezwa kuwa
askari hao wamekuwa wakisafirisha
bangi hiyo mara kwa mara kupitia
mji huo wa Himo bila kukamatwa
kutokana na gari lao kuwa na
namba za kijeshi, hivyo kuwa
vigumu kwa askari wenzao kuwatilia
shaka.

Taarifa zaidi zimedai kuwa
kukamatwa kwa askari hao
kulitokana na gari lao kupata hitilafu
katika eneo hilo la Kilemapofu, na
ndipo askari wa doria walipofika
kwa lengo la kutoa msaada kwa
wenzao, lakini ghafla walisikia
harufu ya bangi.

Mtoa taarifa aliyezungumza kwa
sharti la kutotaka jina lake litajwe,
alisema baada ya askari hao kusikia
harufu ya bangi waliwaarifu viongozi
wao waliowaamrisha walifanyie
upekuzi gari hilo sambamba na
kuwaweka chini ya ulinzi askari wote
waliokuwamo.

Chanzo hicho kiliongeza kuwa katika
upekuzi huo walibaini uwepo wa
magunia 18 ya bangi yaliyolengwa
kupelekwa nchini Kenya.
Kilibainisha kuwa baada askari hao
kukamatwa, mmoja wao alisikika
akiongea na mtu aliyemuita bosi
kumuarifu kukamatwa kwao.

Chanzo hicho kiliongeza kuwa bosi
aliyearifiwa tukio hilo alihoji
imekuwaje wakakamatwa kizembe
namna hiyo.

Kilidokeza kuwa bosi huyo alimhoji
aliyempigia simu kuwa wamebaki na
shilingi ngapi ili wawape rushwa
polisi waliowakamata.

“Bosi aliambiwa kuna laki tano, naye
akawaambia wawape fedha hizo
zote, lakini kwa bahati mbaya
hawakufanikiwa,” kilisema chanzo
chetu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Arusha, Liberatus Sabas, hakukiri
wala kukanusha kuwapo kwa taarifa
za kukamatwa kwa askari wake.

Tanzania Daima lilitaka kujua Jeshi
la Polisi mkoani Arusha limechukua
hatua gani dhidi ya askari hao
ambapo kamanda Sabas alisema
hayupo katika nafasi nzuri ya
kulizungumzia jambo hilo kwa kuwa
yupo hospitalini.