Vikongwe Wauwawa Kwa Kuchomwa Moto

MAUAJI ya kikatili yametokea usiku
wa kuamkia leo wilayani Bunda,
mkoani Mara baada ya watu wenye
hasira wa kijiji cha Kasaula kuwauwa
kwa kuwachinja kama Kuku kisha
kuwachoma moto vikongwe watatu
kwa kuwatuhumu wanajihusisha na
vitendo vya kishirikina.
Pia watu hao mbali na kuwaua
kikatili vikongwe hao kwa tuhuma
kwamba walimuua kijana mmoja
aitwaye Sale Ligolo, walichoma
moto na kuteketeza nyumba
walizokuwa wakiishi wazee hao
pamoja na kupora kuku waliokuwa
wakiwafuga na kuwatafuna kumaliza
hasira zao.

Kwa mujibu wa wa taarifa ya
mwandishi Masau Bwire aliyepo
Bunda kwa sasa, tukio hilo
limetokea usiku wa kumakia leo
baada ya watu hao wenye hasira
kuwasaka ajuza hao baada ya
kuwepo tuhuma kwamba
walishirikiana kumuua kijana huyo
hivi karibuni.

Kijana huyo alikufa kwa kugongwa
na gari, lakini dereva aliyemgonga
alidai hakuona kama alimgonga
mtu ila mbwa na pia inaelezwa
tangu azikwe kijana huyo alikuwa
akirejea kwa mkewe na kumuita
nyakati za usiku pamoja na
kusumbua familia yao akitaka
apewe chakula na ndipo
wanafamilia hao walipoamua
kwenda kwa mganga kuchunguza
tukio hilo.

Wakiwa kwa mganga,wanafamilia
hao walitajiwa majina ya wanakijiji
watatu wa kijiji hicho ambao hata
hivyo walitoroka kwenda vijiji vya
jirani pamoja na familia zao kabla ya
usiku wa leo kuvamiwa
walipokuwepo na kuangushiwa
adhabu hizo za kinyama.
Wa kwanza kushambuliwa na
kuuwa ni bibi aitwaye Bi Mgala
ambaye alikimbilia kijiji cha jiorani
kwa rafiki yake aitwaye Bi Laya,
ambapo walimkata miguu yote
miwili na kumtenganisha kichwa na
kiwiliwili kabla ya kumchoma moto
ambapo hata hivyo kitu cha ajabu ni
kwamba ziliungua nguo zake tu
huku mwili ukiwa upo vile vile.

Baadaye walimgeukia Bi Laya
aliyekuwa akitaka kuwatoroka na
kumfanyia unyama kama rafikie kwa
kosa la kumhifadhi Bi Mgala kwa
kuamini huenda wanafanya
shughuli za kishirikina pamoja na
baadaye kurudi Kasaula na
kumnasa Bi Chausiku na kumfanyia
kama walivyowafanyia ajuza hao
wengine kisha kuchoma nyumba
tatu.

Bibi wa tatu wanayemtuhumu pia
kwa ushirikina, ametimka kijijini
hapo, lakini nyumba yake
imeteketezwa pamoja na kuku
waliokuwa wakiwafuga kuporwa na
watu hao na kutumia moto
waliouwasha katika nyumba hizo
kuwachoma na kuwala kwa hasira.

Kamanda wa Polisi wa Bunda, Mika
David Nyange amethibitisha juu ya
tukio hilo la kusikitisha na kwamba
wanedelea na upelelezi kwa nia ya
kuwasaka waliohusika na kitendo
hicho cha kujichukulia sheria
mikononi.