FBI Watua Arusha

Makachero wa FBI kutoka Marekani
wamewasili nchini Tanzania kusaidia
katika upelelezi wa shambulizi la
bomu lililotekelezwa katika kanisa
katoliki mjini Arusha siku ya jumapili.

Mwandishi wa BBC Baruan Muhuza
akiwa mjini Arusha anasema
makachero hao wa FBI wako Tanzania
kusaidiana na Jeshi la wananchi wa
Tanzania na Polisi kutafuta undani wa
tukio hili ambalo limeishtua na
kuiweka serikali ya Tanzania katika
wakati mgumu.

Baruan Muhuza anaongezea hali
inaonekana kuwa ngumu zaidi hasa
kutokana na aina ya matukio ambayo
yamekuwa yakitokea katika siku za hivi
karibuni yakihusisha viongozi wa dini
ambapo wengi ya wanaodhurika
huwa ni wa imani ya kikristo.

Wakati huo huo wakuu wa serikali
wakishirikiana na viongozi wa kidini
wameandaa mkutano
utakaojumuisha viongozi wapatao
200.

Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam
Said Meck Sadiq amewaambia
wanahabari kuwa wamelazimika
kuandaa mkutano huo wa siku mbili
kufuatia agizo la Rais Jakaya Kikwete.

Mkutano huo utajadili uhusiano bora
baina ya wakrito na waislamu.

Chanzo: BBC