Lipumba Aibua Jambo Zito


MWENYEKITI wa Chama cha
Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim
Lipumba, ameibua suala zito
akikihusisha chama chake na
“kumnusuru” Rais Jakaya Kikwete
katika uchaguzi mkuu uliopita.

Profesa Lipumba alitoboa siri hiyo
katika Msikiti wa Idrissa, Kariakoo,
jijini Dar es Salaam, alikokwenda
kuswali swala ya Ijumaa.
Huku akisisitiza juu ya umuhimu wa
mshikamano wa kiimani, Profesa
Lipumba alianza kwa kuzungumzia
matokeo ya uchaguzi mkuu wa
2010, na ushindani mkali wa kisiasa
uliokuwapo.

Alisema hawaoni matunda ya
jitihada walizofanya kumnusuru Rais
Kikwete asishindwe, kwani hata chini
ya uongozi wake, Waislamu
wameendelea kutothaminiwa.
“Ninyi masheikh mnajua vizuri zaidi
hali ya kisiasa ilivyokuwa, kwamba
ilibidi zifanyike juhudi za makusudi
ili kuokoa jahazi. Lakini pamoja na
kuliokoa jahazi, hali halisi
inaonyesha mpaka sasa hakuna
matunda yoyote yaliyopatikana, na
tupo katika mtihani mgumu zaidi,”
alisema.

Katika hali ambayo inasemekana
ushindi wa Rais Kikwete ulipatikana
kwa mbinu, huku wengine
wakiituhumu Tume ya Taifa ya
Uchaguzi kuwa ilimnusuru
mgombea wa CCM, kauli hii ya
Profesa Lipumba inadokeza kwamba
anajua mkakati zaidi wa kazi ya
Tume ya Uchaguzi.

Katika hali isiyo ya kawaida, Profesa
Lipumba anaonekana kuhamasisha
Waislamu kujipanga akisema
“wenzetu wameanza kujipanga”
kuelekea 2015.
“Kwahiyo kama Waislamu tunataka
kupata haki zetu, kama tunataka
kuishi kama raia wa daraja la
kwanza katika nchi yetu, lazima
tujipange kuelekea uchaguzi mkuu
wa 2015; na sisi tuanze kujipanga
kwa sababu wenzetu wameanza
kujipanga, vinginevyo tutaendelea
kubaki maskini na raia wa daraja la
nne katika nchi yetu wenyewe.

“Mwaka 2010 wakati mshindi wa
uchaguzi wa rais alipotangazwa,
mimi nilikwenda kwenye hafla ya
kutangazwa matokeo, na nilikwenda
makusudi tu, siyo kwamba uchaguzi
ulikuwa huru na wa haki, ila
nilikwenda makusudi kwa kujua hali
ya kisiasa ilivyokuwa wakati huo.

“Huku nilikutana na Sheikh Basaleh.
Nilipokutana naye, alinipongeza;
sijui kama yeye anakumbuka,
akaniambia ‘umeweka mbele imani
yako na umekuwa mwelewa wa
mambo.’”
Hata hivyo, licha ya Profesa Lipumba
kuwaambia Waislamu wajipange
kwa ajili ya uchaguzi mkuu,
hakusema wajipange kupitia chama
kipi.

Lakini alisisitiza kwamba uchaguzi
ujao ni zaidi ya siasa au rais yupi
anafaa, bali maslahi, hasa ya
rasilimali nyeti zinazopatikana katika
ukanda wa Pwani ya Mashariki, eneo
ambalo alisema linakaliwa zaidi na
watu wenye imani ya Kiislamu.

Katika moja ya kauli zake, Profesa
Lipumba alisema kwamba kuna
chama kimoja kinataka kuchukua
madaraka ya nchi, lakini kinasaidiwa
na mataifa ya magharibi, yasiyoenzi
wala kuthamini imani ya Kiislamu.
Kwa muda sasa, zimekuwapo tetesi
kwamba CCM imekuwa inafanya
siasa za udini dhidi ya vyama vya
upinzani, hasa inapoona maslahi
yake yapo hatarini.

Mwaka 2010 makada kadhaa wa
CCM walitumia mitandao ya simu
kuchonga (spoofing) ujumbe wa
simu ulioshambulia mgombea
mmoja wa upinzani, ukimhusisha
na imani yake.

Kauli ya Lipumba imethibitisha pia
minong’ono iliyokuwapo muda
mrefu kuwa baadhi ya kura za
Profesa Lipumba zilipotelea kwa Rais
Kikwete.
Katika uchaguzi huo, Lipumba
alitangazwa kushika namba ya tatu,
nyuma ya Rais Kikwete na Dk.
Willibrod Slaa wa CHADEMA.

Alipoulizwa kuhusu ziara yake
msikitini na kauli aliyotoa, Profesa
Lipumba alikiri kwamba alikwenda
kuzungumzia hali ya kisiasa nchini.

Chanzo:Tanzania Daima