M23 Haiinyimi Tanzania Usingizi yadai Serikali

Tanzania imesema vitisho
vinavyoendelea kutolewa na waasi wa M23
wanaopigana Mashariki mwa Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Congo (DRC), haviinyimi
usingizi.

Hata hivyo, imetaka Jumuiya ya Kimataifa
kutopuuza vitisho hivyo.
Kauli ya Tanzania inakuja huku kukiripotiwa
kuwapo kwa mapigano makali baina ya vikosi
vya Serikali waliopambana na waasi hao, ambao
wameanzisha tena harakati ya kuliteka Jimbo la
Goma na maeneo mengine ya jirani.

Mapigano hayo ni ya kwanza tangu M23,
kuondoka mjini humo mwaka jana kufuatia
shinikizo za kidiplomasia.

Umoja wa Mataifa (UN), umesema utaongeza
kasi ya juhudi zake za kutafuta amani kwa
kutuma kikosi cha wanajeshi 3,000 kujaribu
kuzima mapigano hayo, ambayo yalisababisha
watu 19 kuuawa na wengine kujeruhiwa.

Msemaji wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania
(JWTZ), Kanali Kapambala Mgawe alisema vikosi
vya Tanzania vilivyoko Congo vitaendelea
kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia
weledi na miongozo ya UN.
Kanali Mgawe alisema kauli zozote za vitisho
vinazoendelea kutolewa na waasi hao, haziwezi
kurudisha nyuma juhudi hizo.

Hata hivyo, Kanali Mgawe aliitaka Jumuiya ya
Kimataifa kutopuuzia vitisho hivyo.

“Inawezekana kuna jambo hapa maana kwa nini
Tanzania ipewe vitisho ilhali operesheni hiyo ya
amani inahusisha mataifa mengine?” alihoji
Kanali Mgawe.

Nchi nyingine ambazo zimekubali kutuma wanajeshi wake kupigana na waasi hao ni Malawi na Afrika
Kusini.

Waasi wa M23 wamekuwa wakitoa vitisho kwa wanajeshi wa Tanzania, lakini Serikali imekuwa ikitamba
kuwa hivyo ni vitisho na kazi ya kulinda amani itaendelea kama ilivyopangwa.

Tayari, Katibu Mkuu wa
UN, Ban-Ki Moon ametembelea nchi hiyo.