Babu Wa Loliondo Ashitakiwe

KAMBI rasmi ya upinzani
imeibua upya hoja ya tiba ya
asili maarufu kama Kikombe
cha Babu wa Loliondo, ikihoji
kwamba Serikali haijatoa kauli
wala kuchukua hatua dhidi ya
Mchungaji mstaafu wa Kanisa
la Kiinjili la Kilutheri Tanzania
(KKKT), Ambilikile Mwaisapile
aliyekuwa akitoa tiba hiyo.
Msemaji Mkuu wa kambi hiyo,
Wizara ya Afya na Ustawi wa
Jamii, Dk Antony Mbassa
alihoji jana bungeni katika
hotuba yake kuhusu makadirio
ya mapato na matumizi kwa
mwaka 2013/14.

Alisema kwa mujibu wa
aliyekuwa Waziri wa Afya na
Ustawi wa Jamii, Dk Hadji
Mponda, watu 116 walifariki
dunia kutokana na sababu
mbalimbali wakiwa kijiji cha
Samunge, ilikokuwa ikitolewa
tiba hiyo na mchungaji
Mwaisapile.

“Mpaka leo Serikali haijasema
chochote kuhusu uchunguzi
wa dawa ya babu. Mpaka leo
Serikali haijatoa kauli yoyote
wala kuchukua hatua yoyote
dhidi ya Mzee Mwaisapile
ambaye Februari hii alitoa
kauli nyingine juu ya ugunduzi
wa dawa nyingine,” alisema
Mbassa.

Kwa mujibu wa Mbassa, timu
ya uchunguzi iliyoundwa
mpaka Machi 2011 ilikuwa
imeandaa kukamilisha
taratibu , ili kufuatilia
maendeleo ya kiafya ya
wagonjwa 200 ambao
wamekubali kwa ridhaa yao
kushiriki katika utafiti huo
kuona maendeleo yao kiafya
baada ya kunywa dawa hiyo.

Wakati huo huo, kambi hiyo ya
upinzani imeishauri Serikali
kutoa taarifa rasmi kwa
wananchi juu ya dawa bandia
za kupunguza makali ya
Ukimwi (ARVs) makopo 4,000,
ambazo hazijakusanywa ili
kuwaondolea mashaka na
kuwajengea imani watumiaji.

Kambi hiyo imesema sakata la
kuwepo ARVs bandia
lililochukua miezi minane sasa,
limekuwa na sura tofauti
hususan juu ya nani anahusika
moja kwa moja baada ya
kiwanda cha Tanzania
Pharmaceticals Industry (TPI),
kukanusha kuhusika wakati
Mamlaka ya Chakula na Dawa
(TFDA) na Bohari Kuu (MSD )
wakisisitiza zimetoka
kiwandani hapo.

“Wakati taratibu za kitaalamu
na kisheria zikiendelea
tunaishauri Serikali kutoa
taarifa rasmi kwa wananchi
juu ya dawa ambazo
hazijakusanywa. Je, ziko
vituoni au zilishatumiwa na
wananchi? Kama
zilishatumiwa, je, serikali ina
taarifa zozote juu ya
waliozitumia dawa hizo? Je,
kuna madhara yoyote
waliyoyapata kutokana na
kuzitumia,” alisema.

Kulingana na taarifa ya kambi
ya upinzani, jalada la kesi ya
ARVs bandia limepokewa na
linashughulikiwa na
Mkurugenzi wa Mashitaka
(DPP) ili kupata mwelekeo wa
nani ahusishwe na kwa kosa
gani kabla ya kuachia mamlaka
husika jukumu la uchunguzi
wa kina.

Taarifa hiyo ya kambi inasema
ofisi ya DPP ilitoa maelezo
kwamba suala hilo limechukua
muda mrefu wa zaidi ya miezi
miwili tofauti na muda wa
kawaida wa siku 14
unaotumiwa na ofisi hiyo
kushughulikia kesi mbalimbali
zinazofikishwa kutokana na
uzito na unyeti wa suala hilo.