Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim
Poulsen leo (Mei 16 mwaka huu)
ametaja kikosi cha wachezaji 26
watakaoingia kambini kujiwinda kwa
mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia
dhidi ya Morocco itakayochezwa Juni 8
mwaka huu jijini Marrakech, Morocco.
Katika kikosi hicho, Kim ameita
wachezaji wapya sita ingawa baadhi
yao wamewahi kuchezea timu hiyo,
huku akiacha wengine watatu aliokuwa
nao kwenye mechi ya kwanza dhidi ya
Morocco ambapo Taifa Stars ilishinda
mabao 3-1.
Wapya aliowaita katika kikosi hicho
kitakachoingia kambini Mei 20 mwaka
huu, saa 1 jioni kwenye hoteli ya
Tansoma jijini Dar es Salaam ni Ally
Mustafa, Vicent Barnabas, Juma Luzio,
Haruna Chanongo, Mudhathiri Yahya
na Zahoro Pazi. Wachezaji aliowaacha
ni Shabani Nditi, Nassoro Masoud
Cholo na Issa Rashid.
Kikosi kamili cha Taifa Stars
inayodhaminiwa na Kilimanjaro
Premium Lager ambacho kabla ya
kwenda Morocco kitapita jijini Addis
Ababa, Ethiopia kucheza mechi ya
kirafiki Juni 2 mwaka huu dhidi ya
Sudan ni kama ifuatavyo;
Makipa ni nahodha Juma Kaseja
(Simba), Aishi Manula (Azam), Ally
Mustafa (Yanga) na Mwadini Ally
(Azam). Mabeki ni Aggrey Morris
(Azam), Erasto Nyoni (Azam), Kelvin
Yondani (Yanga), Nadir Haroub
(Yanga), Shomari Kapombe (Simba),
Vicent Barnabas (Mtibwa Sugar) na
Waziri Salum (Azam).
Viungo ni Amri Kiemba (Simba),
Athuman Idd (Yanga), Frank Domayo
(Yanga), Haruna Chanongo (Simba),
Khamis Mcha (Azam), Mwinyi Kazimoto
(Simba), Mudathiri Yahya (Azam) na
Salum Abubakar (Azam).
Washambuliaji ni John Bocco (Azam),
Juma Luzio (Mtibwa Sugar), Mbwana
Samata (TP Mazembe, Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Congo- DRC), Mrisho
Ngasa (Simba), Simon Msuva (Yanga),
Thomas Ulimwengu (TP Mazembe,
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo-
DRC) na Zahoro Pazi (JKT Ruvu).
Kocha Kim amesema kikosi
kitakachoingia kambini kitakuwa na
wachezaji 24 ambapo Samata na
Ulimwengu watajiunga na timu jijini
Marrakech, lakini wachezaji
atakaondoka nao Dar es Salaam
kwenda Addis Ababa ni 22 ambapo
ataacha kipa mmoja na mchezaji
mmoja wa ndani.
Awali TFF ilikuwa imeitafutia Taifa Stars
mechi ya kirafiki Juni 1 mwaka huu
dhidi ya Algeria, Libya au Misri. Lakini
baadaye Algeria ikasema itacheza na
Togo, wakati Misri ilitaka mechi hiyo
ichezwe Juni 4 jijini Cairo, jambo
ambalo lisingewezekana kwa Stars
kwani ina mechi ya mashindano Juni 8
mwaka huu.
Kwa upande wa Libya mechi hiyo
ilikubaliwa ichezwe Tunis, Tunisia, Juni
2 mwaka huu.
Lakini baadaye Libya
ikataka mechi hiyo ichezewe jijini Tripoli
ambapo TFF ilikataa kutokana na
sababu za kiusalama.
TANZANIA YAJIONDOA MICHUANO YA
COSAFA
Tanzania (Taifa Stars) imejitoa kwenye
michuano ya Baraza la Vyama vya
Mpira wa Miguu Kusini mwa Afrika
(COSAFA) itakayofanyika nchini Zambia
kuanzia Julai 2-26 mwaka huu.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF), Angetile Osiah
amesema Stars ambayo iliingizwa katika
michuano hiyo kama timu mwalikwa
imejitoa kutokana na mwingiliano wa
ratiba kati ya michuano hiyo na mechi
za Kombe la Afrika kwa Wachezaji wa
Ndani (CHAN).
Amesema awali Tanzania ilithibitisha
kushiriki michuano kwa matarajio
kwamba Uganda ingekubali ombi la TFF
la kubadilisha ratiba ya mechi za CHAN,
lakini Shirikisho la Mpira wa Miguu
Uganda (FUFA) likagoma kwa vile
kipindi ambacho kilipendekezwa
lenyewe litakuwa na uchaguzi wa
viongozi wao.
Taifa Stars itacheza na Uganda (The
Cranes) katika mechi za CHAN ambapo
mechi ya kwanza itachezwa jijini Dar es
Salaam kati ya Julai 12-14 mwaka huu
wakati ya marudiano itafanyika jijini
Kampala kati ya Julai 26-28 mwaka huu.
Akizungumzia michuano ya COSAFA,
Kocha Kim amesema angependa
kushiriki michuano hiyo kwani
ingekuwa kipimo kizuri kwa kikosi
chake, lakini kwa sasa malengo
makubwa ya Stars kwenye mechi za
mchujo za Kombe la Dunia na
michuano ya Kombe la Mataifa ya
Afrika (AFCON) ambayo fainali zake
zitafanyika mwaka 2015.