Polisi Wa Bangi Atoroka

JESHI la Polisi mkoani Arusha linamshikilia ofisa wa jeshi hilo, Inspekta Isaac Manoni, kwa
tuhuma za kumtorosha mtuhumiwa wa usafirishaji wa magunia ya bangi, Koplo Edward.

Koplo Edward ni dereva wa gari la polisi lenye namba za usajili T 2025, aina ya Toyota Land
Cruiser, linalodaiwa kutumika kubeba magunia 18 ya bangi.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alisema jana kuwa katika sakata la
usafishaji wa bangi kwenda Holili, mpakani Kenya, watuhumiwa walikuwa wawili, akiwamo
askari namba G. 2434, PC George, ambao wote wamefukuzwa kazi.

Hata hivyo, habari zaidi zinasema kuwa kutoroka kwa askari huyo kunadaiwa kuwa ni mpango
uliotengenezwa na askari wenzake ili kupoteza ushahidi katika kashfa hiyo.

Inaelezwa kuwa askari huyo aliwatoroka askari waliokuwa wakimlinda akiwa nyumbani kwake
baada ya kuwahadaa kuwa anachukua pesa na ndipo alipotokea mlango wa nyuma.

Baadhi ya askari mjini Moshi waliozungumza kwa sharti la kutotaka majina yao yatajwe,
walidai kuwa tukio hilo ni mpango uliosukwa na baadhi ya askari wenzake wa Arusha kwa
lengo la kumwepusha na balaa mmoja wa vigogo wa jeshi hilo anayedaiwa kuwa kwenye
mtandao wa kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi.

Askari huyo ndiye anayedaiwa kumpigia simu kigogo mmoja wa polisi mjini Arusha
akimtaarifu kukamatwa kwao na akakaripiwa kwa kukamatwa kizembe huku mpango wa
kuwapa rushwa askari wa doria waliowakamata ukikwama.

“Wakati wakiwa katika nyumba ya mtuhumiwa huyu kulikuwa na askari saba, akiwamo
Inspekta. Isaac ambaye alikuwa kiongozi, hivyo baada ya tukio lazima tumshikilie huyu kwa
uzembe kazini,” alisema kamanda huyo.

Awali watuhumiwa hao walikamatwa Mei 18, mwaka huu, majira ya saa 5 usiku huko Himo na
askari polisi wa Kilimanjaro wakiwa na gari la polisi lenye namba za usajili T 2025, Toyota Land
Cruiser lililokuwa likiendeshwa na Koplo Edward huku likiwa na magunia 18 ya bangi
yakipelekwa Holili, mpakani Kenya.

Hata hivyo jeshi hilo limetoa wito kwa mtu yeyote anayefahamu mahali alikotorokea
mtuhumiwa huyo atoe taarifa polisi na kuwafichua watu wote wenye mtandao wa biashara
haramu ya bangi.

Kamanda Sabas alisema kuwa tayari ameshatoa taarifa kwa vyombo vya habari juu ya
kutoroka kwa askari huyo na hatua zilizochukuliwa kwa askari waliokuwa wakimlinda, hivyo
hawezi kutoa taarifa nyingine kwa njia ya simu.
Katika hatua nyingine, askari PC George, mwenye namba za usajili G. 2434 amefikishwa
mahakamani mkoani Kilimanjaro.

Mbali na askari huyo, pia mfanyabiashara mmoja, Livingstone Urassa, wa Usseri Wilaya ya
Rombo alifikishwa mahakamani pamoja na askari huyo ambapo wote walisomewa shitaka la
kula njama na kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi.

Washtakiwa hao walifikishwa mbele ya Hakimu Simon Kobelo, ambaye ni Hakimu Mkazi
Mfawidhi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mjini Moshi.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka iliyosomwa na wakili wa serikali, Abdallah Chavula,
washtakiwa hao wanadaiwa kuwa siku, muda na mahali pasipofahamika walikula njama ya
kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi.

Shitaka la pili lilimhusu PC George, ambaye anadaiwa kuwa Mei 18, mwaka huu huko Kilema,
Wilaya ya Moshi, mshtakiwa alisafirisha dawa za kulevya aina ya bangi magunia 18, ikiwa na
thamani ya sh milioni 81.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 5, mwaka huu itakapokuja kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa
hawakutakiwa kujibu chochote kutokana na mahakamana hiyo kutokuwa na uwezo wa
kusikiliza shauri hilo.


Chanzo:freemedia.com