Taarifa toka Ikulu Juu ya Kauli ya Dr. Slaa

KATIBU Mkuu wa Chama
cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA), Mheshimiwa
Wilbroad Slaa, Jumatatu, Mei 13,
2013, amekaririwa na gazeti moja
akidai kuwa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Jakaya Mrisho
Kikwete na timu yake ya kampeni,
“ilikuwa ikisaka kura kwenye
nyumba za ibada na kumwaga
sumu mbaya ya udini ambayo
sasa inaitesa Serikali na taifa”
kwenye Kampeni za Uchaguzi
Mkuu wa 2010.

Aidha, katika habari hiyo
iliyoandikwa chini ya kichwa cha
habari, “Dk. Slaa amlipua JK”
kwenye gazeti linalounga mkono
CHADEMA la Tanzania Daima,
Mheshimiwa Slaa anadai kuwa
migogoro ya sasa ya kidini
“inajengwa au kutengenezwa na
Serikali iliyojikita kusambaza
sumu ya udini katika misikiti
wakati wa kampeni za Urais
mwaka 2010” .

Kwa hakika, hakuna
namna nyingine ama namna bora
zaidi ya kuielezea kauli hii ya
Mheshimiwa Slaa isipokuwa
kwamba kauli hiyo ni riwaya
nyingine isiyokuwa na mshiko. Ni
uongo mtupu. Yake Mheshimiwa
Slaa ni maneno yasiyokuwa na
ukweli wowote. Ni uzushi na
santuri ambayo imezoeleka sasa
kwa wananchi.

Kauli ya Mheshimiwa Slaa
ni mwendelezo wa mtiririko
usiokuwa na mwisho wa ghiriba
ambazo kamwe hazitafanikiwa za
Mheshimiwa Slaa kuwahadaa
wananchi kuhusu ukweli wa
mambo ulivyo katika nchi yetu.

Rais Jakaya Mrisho
Kikwete na timu yake ya kampeni
kamwe hawakufanya kampeni za
Uchaguzi Mkuu wa 2010, ama wa
mwaka mwingine wowote, katika
nyumba yoyote ya ibada iwe
msikitini ama kanisani ama
hekaluni ama nyumba nyingine
yoyote ya ibada mahali popote
katika nchi yetu.
Mheshimiwa Rais Kikwete
hajawahi hata kufikiria
kuchanganya dini na siasa. Hana
sababu ya kufanya hivyo.

Anaelewa fika madhara ya udini
kwa mustakabali wa nchi yetu,
kwa umoja wa taifa letu na kwa
mshikamno wa wananchi wake.

Yoyote anayejaribu kumbebesha
Rais Kikwete msalaba wa udini
ana lake jambo na ni vyema
atuambie fika Rais alitumia
Msikiti upi, ama Kanisa lipi,
mahali gani na kwa nyakati gani
kufanya kampeni.

Vinginevyo, kauli ya
Mheshimiwa Slaa itabakia ni kauli
tu inayostahili kupuuzwa na
wananchi, itabakia ni kauli ya mtu
mzima anayetapatapa na kufanya
jitihada kubwa kujivunjia mwenye
heshima kwa kutunga na
kusambaza uongo.
Tunanapenda kumshauri
Mheshimiwa Slaa kuwa kama hana
jambo la maana la kuwaambia
wananchi ama ameishiwa na hoja
ni vyema anyamaze, awaachie
wananchi waendelee na shughuli
zao za maendeleo, kuliko
kuendeleza riwaya zake
zisizokuwa na mshiko. Yake ni
santuri iliyowachosha wananchi.

Imetolewa na :
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
13 Mei, 2013