Saigon Waponea ChupuChupu Kwa Warriors

Timu ya Saigon kutoka mkoani kigoma hii leo wameponea chupuchupu kuchezea kichapo kutoka kwa Katavi Warriors ya mkoani Katavi.

Katika uwanja wa Lake Tanganyika Saigon wamefanikiwa kutumia uwanja huo wa nyumba vizuri kwa kuibuka na ushindi wa taabu wa goli tatu kwa mbili.

Kipindi cha kwanza kiliisha kwa kila timu kutoona lango la mwenzie, Walikuwa ni Warriors katika kipindi cha pili walipoanza kupata goli kabla ya Saigon kusawazisha dakika chache baadae.

Aston Villa kama wanavyofahamika katika mitaa ya Majengo, kawajense na viunga vyote vya Mpanda hawakufanya ajizi tena walipopachika goli la pili na kufanya matokeo kusomeka 1-2. Wazee wa mikebuka walirudi kwa spidi na kusawazisha goli hilo na dakika chache kuongeza goli la tatu.

Mchezo wa marudioano utafanyika katika Uwanja wa Azimio katikati ya mji wa Mpanda mkoani Katavi siku ya Jumapili tarehe 2 June. Kabla ya mchezo huo Warriors watapambana na Rhino Rangers kutoka Tabora katika uwanja wa Azimio, mchezo huo ni wakujipima nguvu.

Katavi Warriors wanahitaji ushindi wa goli moja kwa bila ili kuweza kujihakikishia nafasi ya kusonga mbele katika michuano hii ya kuelekea ligi daraja la pili. The Warriors wamefika hapo baada ya kuwaondosha Rukwa United na Saigon kuwafungashia virago Mirambo ya Tabora.