Tamko La Rais Jakaya Kikwete Juu Ya Mlipuko Wa Arusha

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Jakaya
Mrisho Kikwete amepokea kwa
mshtuko na masikitiko makubwa
taarifa ya tukio la leo, Jumapili, Mei
5, 2013 la mlipuko kwenye Kanisa
Katoliki la Mt. Joseph Mfanyakazi la
Olasiti Jijini Arusha.

Tukio hilo la
kigaidi limesababisha mtu mmoja
kupoteza maisha na wengine 40
kujeruhiwa. Rais Kikwete analaani
vikali shambulio hilo lililofanywa na
mtu au watu katili, waovu na wenye
dhamira mbaya na nia mbaya kwa
Tanzania na watu wake.

Rais Kikwete ameagiza vyombo vya
usalama nchini kumsaka mtu au
watu waliohusika na kitendo hicho
kiovu na kuwafikisha kwenye
vyombo vya sheria.

Vile vile Rais
Kikwete amewataka wananchi wote
kuwa watulivu wakati Serikali na
vyombo vyake inaendelea kufuatilia
tukio hili. Tutawasaka popote walipo
na kupambana nao bila huruma.

Aidha, tutakabiliana na aina yoyote
ya uhalifu nchini iwe ni ugaidi au
aina yoyote ya uhalifu wa namna
hiyo au wa namna nyingine, uwe na
chimbuko lake ndani ya nchi ama
nje ya nchi yetu.

Kamwe
hatutakubali kuwaacha wavuruge
amani na usalama wa Tanzania na
watu wake. Rais anaamini kuwa
Serikali, kwa msaada na ushirikiano
wa wananchi, watu hao
watapatikana na kuadabishwa
ipasavyo.

Aidha, Rais Kikwete anatoa
rambirambi za dhati ya moyo wake
kwa wafiwa na wale wote ambao
wamejeruhiwa katika tukio hilo.
Anaungana nao katika machungu
na msiba.

Rais pia anawaombea
wote walioumia katika tukio hili
wapate nafuu ya haraka na
waendelee na shughuli zao za
ujenzi wa taifa.

Rais Kikwete vilevile anatoa pole
nyingi kwa viongozi na waumini wa
Kanisa Katoliki kwa tukio hili la
kusikitisha na kuvurugika kwa ibada
na shughuli yao muhimu ya
uzinduzi wa Kanisa lao.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
IKULU,
DAR ES SALAAM
5 Mei, 2013