Mwalimu Ajifungua Watoto Watano

Mwalimu wa Shule ya Sekondari
Luwawasi iliyopo Manispaa ya Songea, Sophia
Mgaya (28) amejifungua kwa njia ya upasuaji
watoto watano jana asubuhi katika Hospitali ya
Rufaa ya Songea ambapo watatu kati yao ni wa
kiume na wawili wa kike.

Upasuaji huo ambao umefanywa na Daktari
Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake, Dk Mgonde
umefanyika kwa mafanikio ambapo ulifanywa
saa 5:15 asubuhi na kumalizika 5:45 asubuhi
baada ya Mwanamke huyo kugundulika akiwa
na tatizo la kutanguliza kitovu wakati ujauzito
wake ukiwa na miezi saba.

Akizungumza na waandishi wa habari jana
katika wodi ya wajawazito hospitalini hapo,
Ofisa muuguzi msaidizi Vilgilia Mselewa
amesema, walimpokea mama huyo jana saa 6
mchana baada ya kufanyiwa upasuaji na hali
yake pamoja na wanawe inaendelea vizuri.

Amesema, mtoto wa kwanza ni wa kike
amezaliwa akiwa na gramu 730, mtoto wa pili ni
wa kiume  ana uzito wa gramu 810, watatu wa
kiume alikuwa na gramu 670 wanne wa kiume
gramu 820 na watano ni wa kike aliyekuwa na
gramu 430, hali za wototo zinaendelea vizuri na
wapo kwenye chumba cha watoto ambao
hawajatimiza miezi.
Akizungumza hospitalini hapo na Mwananchi,
Mama mzazi wa watoto hao, amesema
amefurahi kupata watoto hao na anamshukuru
Mwenyezi Mungu kwa upendo mkubwa
aliompatia kwani alilia sana alipopoteza
mwanaye wa kwanza wa kike aliyezaliwa
mwaka 2010 na kufariki akiwa na miezi saba.

Aidha amewashukuru madaktari na wauguzi
kwa msaada walimpatia kwani bila wao hali
ingekuwa mbaya na amewataka Watanzania
kuendelea kumwombea yeye na wanaye ili aweze kupata afya njema na kuweza kuwalea watoto wake
kwani ana hamu ya kuwaona wakikua na kuendelea kumfariji katika maisha yake.

Naye baba mzazi wa watoto hao Zacharia James (30) mkazi wa Mkoa wa Njombe amemshukuru Mungu.

Chanzo: Mwananchi.