Majambazi Waiba Kanisani.

KATIKA hali isiyokuwa ya
kawaida, usiku wa kuamkia
jana majambazi waliangusha
mfuko wa mamilioni ya fedha
na simu mbili makaburini
wakati wakiwakimbia polisi
baada ya kuvamia, kuvunja na
kuiba fedha hizo katika Kanisa
Katoliki la Mtakatifu Francisco
wa Sales Parokia ya Mkuza,
Jimbo Kuu la Dar es Salaam,
Kibaha mkoani Pwani.
Katika tukio hilo lililotokea
saa tisa usiku, Polisi walipiga
risasi juu baada ya kupewa
taarifa na majirani, na
kuwafanya majambazi hao
waliokuwa tisa, kutimua mbio
kwa kuruka ukuta upande wa
makaburini na kuangusha
mfuko wenye fedha zaidi ya Sh
milioni tatu, fedha za kigeni na
simu mbili.

Paroko wa kanisa hilo, Padri
Mathew Chavely aliliambia
gazeti hili jana kuwa,
majambazi hao walivunja
mlango wa ofisi baada ya
kuwafunga kamba walinzi na
kuwawekea plasta midomoni
kisha kufanikiwa kuiba fedha
hizo.

“Tulijua wakitoka ofisini,
wanatujia sisi nyumbani, ila
kabla, watu wema walitoa
taarifa polisi na mara polisi
wakaja hapa, walipiga risasi
wale wezi wakakimbia na
fedha zote, asubuhiwakati wa
uchunguzi, kumbe
waliangusha fedha makaburini,
karibu na kanisa,” alisema
Padri Chavely.

Alipoulizwa kwa nini wakae na
fedha nyingi ofisini, Padri
Chavely alisema kanisani hapo
hivi sasa wanaendelea na
ujenzi wa kanisa jipya kubwa,
hivyo Jumapili ya juzi, mbali ya
kukusanya sadaka za kawaida,
kulikuwa na harambee ya
ujenzi wa kanisa hilo.

Padri Chavely aliwashukuru
waumini na majirani kwa sala
na kutoa taarifa polisi na
aliwaombea majambazi hao
wabadilike, wamrudie Mungu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Pwani, Ulrich Matei
alithibitisha kutokea kwa
tukio hilo na kueleza kuwa,
asubuhi walimshikilia Karani
wa Ofisi, Deus Cosmas kwa
mahojiano, lakini walimuachia
baada ya kupata simu mbili za
majambazi hao
zilizodondoshwa makaburini
pamoja na fedha zote.
“Ni kweli saa tisa usiku leo
(jana) walivamia kanisa hilo,
wezi waliokuwa tisa, wakiwa
na silaha za jadi kama
marungu, mapanga, nyundo na
nyinginezo, tulipopata taarifa
tulifika mara moja na kwa
kuwa hatukujua walioko ndani
wana silaha gani zaidi,
tuliamua kupiga risasi juu,
ndipo walipokimbia kwa
kuruka ukuta nyuma, eneo la
makaburini,” alisema Kamanda
Matei.

Akielezea zaidi tukio hilo,
Kamanda Matei alisema wezi
hao waliwafunga kamba na
plasta walinzi kabla ya
kuvunja ofisi ya kanisa na
kuiba Sh 3,172,450, Dola za
Marekani 13, fedha za Uganda
Sh 18,700, fedha za Kenya Sh
200 na Rupia 328.

Kwa mujibu wa Polisi,
kutokana na ukubwa wa eneo
hilo, majambazi walitumia
ukuta wa nyuma kuruka na
kukimbia na wakati
wakikimbia, katika eneo hilo
lenye makaburi, walikuta
damu kwenye misalaba kadhaa
iliyoharibiwa kwa
kupindishwa na kutokana na
purukushani hiyo, waliangusha
mfuko wenye fedha zote
walizoiba na simu hizo mbili.

Kamanda Matei alisema
usalama umeimarishwa eneo
hilo, na kupitia simu hizo, kwa
kutumia Teknolojia ya Habari
na Mawasiliano (Tehama),
wamebaini mtandao na
mambo mengi ambayo
yatawawezesha kuwakamata
wote wanaohusika na tukio
hilo na matukio mengine
mkoani humo.

Chanzo:Habarileo