Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete
leo amekutana na timu ya Taifa (Taifa
stars) kwa lengo la kuitia moyo katika
mechi ijayo kati yake na timu ya Moroco
ikiwa ni harakati za Tanzania kutafuta
tiketi ya kucheza fainali za kombe la Dunia
kwa mara ya kwanza mwaka 2014.
Rais Kikwete ameiambia timu hiyo kuwa
ina uwezo mkubwa wa kusonga mbele
kutokana na uwezo mkubwa waliouonesha
katika mchezo wao dhidi ya Gambia
ambapo walifanikiwa kupata ushindi wa
bao 2-0.
“Maadamu mara ya kwanza mliwashinda
Gambia, hakikisheni pia mnapata ushindi
dhidi ya Moroco, mkishinda tunafurahi
sana na mkishindwa tunanyong’onyea
sana,” amesema Rais Kikwete.
Aidha amempongeza kocha wa timu hiyo
Kim Poulsen pamoja na Kamati ya Taifa
ya ushindi ya Taifa stars kwa kuisaidia
timu hiyo kiasi cha shilingi milioni 30
ikiwa ni mkakati wa kuiongezea nguvu
kwa hatua iliyofikia na kuwataka
wachezaji kujituma ili kuwafurahisha
watanzania ambao hivi sasa wanaipenda
timu yao ya Taifa.
Nae Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni
na Michezo Fenera Mukangara amesema
Serikali itaendelea kushirikiana na wadau
mbalimbali wa michezo nchini ili kuondoa
changamoto zinazoikabili timu hiyo.
Kwa upande wake Kocha Poulsen,
amemshukuru Rais Kikwete kwa
kuwakaribisha na kuwatia moyo ambapo
ameahidi kuifundisha vizuri timu hiyo ili
kuhakikisha kuwa wanapata ushindi.
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji
wenzake kaptaini wa timu hiyo Juma
Kaseja amemshukuru Rais Kikwete na
kuahidi kujituma kwenye mazoezi na
hatimaye kuibuka washindi kwenye mechi
zijazo.
Taifa stars ambayo inakamata nafasi ya
pili katika kundi C inatarajia kucheza
ugenini na Morocco mnamo Juni 7 mwaka
huu.