Vatican Wa Wasilisha UN taarifa ya Bomu Arusha

Tukio la kutupwa bomu katika
Kanisa Katoliki la Joseph
Mfanyakazi, Arusha limetua katika
Baraza la Usalama la Umoja wa
Mataifa (UN) baada ya kuwasilishwa
na Balozi wa Vatican UN, Askofu
Mkuu Frances Chullikatt. Askofu
Chullikatt anakuwa kiongozi wa
kwanza wa Vatican kutoa tamko
kuhusiana na shambulizi hilo
ambalo mmoja wa viongozi wake
alikuwapo.

Bomu hilo lilirushwa katika kanisa
hilo wakati likizinduliwa na Balozi wa
Vatican nchini, Askofu Mkuu
Francisco Padilla Mei 5, mwaka huu
na kusababisha vifo vya watu
watatu na kujeruhi zaidi ya 50.
Wakati wa shambulizi hilo, Askofu
Padilla na Askofu Mkuu wa Jimbo la
Arusha, Josephat Lebulu
walionusurika.

Akihutubia Kikao cha Baraza la
Usalama la Umoja wa Mataifa, New
York, Marekani juzi, Askofu
Chullikatt alisema tukio lililotokea
Arusha linadhihirisha kuwa kuna
umuhimu ya kupambana na ugaidi
katika Afrika ili kuimarisha amani na
usalama wa kimataifa.“Unahitajika
mshikamano na ushirikiano wa
pamoja wa mataifa mbalimbali
katika kuchukua hatua za maisha na
kulinda haki za binadamu,” alisema
Askofu Chullikatt, ambaye amekuwa
mwakilishi wa Vatican kwenye
Umoja wa Mataifa tangu mwaka
2010.

Askofu Chullikatt, ambaye ni
mzaliwa wa India, alisema suala la
ugaidi linahitaji kuzuiwa duniani
kote na hasa Afrika kutokana na
matukio hayo kuharibu maisha ya
binadamu na kutokea katika
maeneo wanayofanyia ibada.

Askofu Chullikatt alisema pale ugaidi
unapofanyika kwa kutumia dini,
waumini na viongozi wao ni lazima
wahakikishe wanapambana nao ili
kuutokomeza.

Alisema suala la ugaidi linahitaji
viongozi wa kisiasa, kijamii na kidini
kulilaani kwani ni la kikatili katika
maisha ya binadamu hivyo si vyema
kukaa kimya suala hilo linapotokea.

Askofu Chullikatt alisema ugaidi
unaotokea Afrika unatakiwa
kuangaliwa kimataifa ili kuzipa
uwezo nchi hizo kupambana na
kuzuia matukio hayo.

Shambulio la bomu dhidi ya kanisa
la Arusha lilikuwa tukio la pili la
ugaidi uliolenga kushambulia
wageni nchini.

Mara ya kwanza
ilitokea mwaka 1998, wakati Ubalozi
wa Marekani nchini ulipolipuliwa
kwa bomu na kusababisha vifo vya
watu kumi na moja huku 85
wakijeruhiwa.