Obama Ajipanga Ziara ya Afrika

Rais wa Marekani Barack Obama
anatarajiwa kuzuru Senegal, Afrika
Kusini na Tanzania mwezi Juni. Hii ni
kwa mujibu wa taarifa kutoka ikulu ya
White house.

Rais Obama atakutana na watunga
sheria na wafanyabiashara pamoja na
viongozi wa asasi za kijamii.

Ziara ya Obama itaanza tarehe 26 Juni
hadi 3 Julai na itakuwa ziara yake ya
pili Kusini mwa jagwa la Sahara akiwa
rais wa Marekani.
Alizuru Ghana mwaka 2009 .

Rais wa zamani wa Marekani Bill
Clinton na mwenzake George W Bush,
wote walizuru Afrika wakati wa
muhula wao wa pili wa utawala.
Clinton alizuru nchi sita wakati Bush
akizuru nchi tano.

''Rais atatilia mkazo uhusiano kati ya
Marekani na baadhi ya nchi za kiafrika
ambazo zinakuwa ikiwemo maswala
kama ukuwaji wa uchumi, uekezaji na
biashara pamoja na kukuza taasisi za
kidemokrasia na kuendelea kukuza
viongozi wa kizazi kijacho Afrika,''
ilinukuu taarifa kutoka ikulu ya White
House.

Ziara ya Obama pia itatilia mkazo
kukuza uhusiano kati ya Marekani na
watu wa bara la Afrika ili kuendeleza
ushirikiano wa kikanda, amani na
ukuwaji.

Wadadisi wanasema kuwa ziara kama
hizi hufanywa sana na marais wa
Marekani hasa baada ya kuondokewa
na kazi ngumu ya kampeini za
uchaguzi na shinikizo za ndani ya
nchi.

Wakati huohuo, tisho linaloongezeka
kutoka kwa wapiganaji wa kiisilamu
nchini Mali, limefanya kanda hiyo
kumulikwa zaidi na Marekani. Bi
Michel Obama ataambatana na
mumewe katika ziara hiyo.