WAASI WAKUBALI MAFUTA KUUZWA

Makubaliano yameafikiwa kuondoa kizuizi cha kusafirisha mafuta mashariki mwa Libya.

Mauzo ya mafuta katika nchi za ng'ambo nchini humo yaliathirika pakubwa katika kipindi cha miezi minane iliyopita baada ya kufungwa kwa bandari zilizo katika eneo la mashariki linalotawaliwa na makundi ya wanamgambo.

Katika mkutano wa waandishi wa habari uliofanyiwa katika jiji la Beghazi, Waziri wa Maswala ya Haki wa Libya, Salah Al-Maghani, alithibitisha kuondolewa kwa muda kwa vizuizi vya kuuza mafuta.

Vituo vya mafuta vya Hureiga na Zuetina vilivyo na uwezo wa kuzalisha mafuta mapipa 200,000kwa siku hivi sasa vimesimamiwa na Serikali.

Vituo viwili vilivyo vikubwa zaidi nchini humo vya Mashariki mwa nchi vya Ras Lanuf na Sidra vitafunguliwa kwa muda wa majuma machache yajayo, kulingana na Waziri.

Mapatano yaliafikiwa kati ya makundi ya wapiganaji yaliyosababisha kufungwa kwa vituo hivyo na kundi ambalo Serikali ililitaja kama"wapatanishi".

Msemaji wa Waziri Mkuu ameambia BBC kuwa Serikali imekubali kuwalipa mishahara walinzi wa vituo hivyo vya mafuta.

Juhudi za mwezi uliopita za kufikia mapatano ya kuanza kuuza mafuta tena katika vituo hivyo hazikufaulu.

Wale wanaozuia mafuta kuuzwa katika vituo hivyo wamekuwa wakilalamika kuwa sekta ya mafuta nchini Libya inakabiliwa na ufisadi mkubwa, lawama ambayo imekanushwa na maafisawa Serikali.

Wapiganaji hao pia wamekuwa wakisema kuwa wakaazi wa Mashariki wanahitaji mapato makubwa zaidi kutoka kwa mauzo ya mafuta. Waziri wa Haki sasa anasema kuwa Serikali itachunguza lawama za ufisadi.

Libya imepata hasara ya zaidi ya Dola Bilioni tisa tangu kufungwa kwa vituo hivyo vya mafuta. Eneola Mashariki ndilo linalozalisha kiwango kikubwa cha mafuta.