Kutokana na kazi hiyo, jibu la ama Tanzania kuwa na mfumo wa Serikali tatu kama ilivyopendekezwa kwenye rasimu ya pili ya Katiba iliyowasilishwa bungeni hapo na aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba wiki mbili zilizopita, au aina nyingine ya muundo, litapatikana Ijumaa.Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta aliwaambia wajumbe wa Bunge hilo jana kwamba kazi hiyo ya kuchambua sura hizo inafanyika leo na kesho.
Hata hivyo alisema kazi hiyo ingeweza kuanza kufanyika jana kwa kamati ambazo zilikuwa tayari kufanya hivyo. Alisema siku ya janahaikuhesabika kama siku rasmi ya mjadala kutokana na kuwepo shughuli nyingi za kiutawala.Miongoni mwa shughuli hizo ni pamoja na wajumbe kuelekezwa juu ya mfumo wa mjadala kwenye kamati na pia muundo wa uandishiwa sura hizo kuweka mfumo ambao hautaleta tabu katika uandishi wa Katiba mpya.
Kutokana na hali hiyo, Sitta alisema sura hizo zitajadiliwa kwa siku mbili hadi kesho na Alhamisi itakuwa maalumu kwa Kamati ya Uandishi kufanya kazi yake ya kuandika masuala yaliyojadiliwa na kuafikiwa au kutoafikiwa na wajumbe walio wengi.
Ijumaa, wenyeviti wa kamati hizo watawasilisha taarifa zao bungeni kwa mjadala.
Sitta alisema Kamati ya Uongozi ya Bunge Maalumu iliamua kuanza kujadiliwa kwa sura namba moja na sita kutokana na sura hizo kuwa na mambo yanayofanana kuhusu muundo wa Serikali na Muundo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kupatikana kwa muundo kumeelezwa na Mwenyekiti huyo kwamba kutafanya mjadala juu ya masuala mengine kuwa rahisi. "Kama mnavyojua sura namba moja, sura namba sita na sura namba nane zina masuala yanayofanana.
Lakini kwa vile kanuni zinatutaka tujadili sura mbili mbili tutaanza na sura namba moja na sura namba sita ambazo zinafanana maana zinazungumzia muundo wa Jamhuri na Muungano.
"Kamati zitakapojadili kuhusu muundo wa Serikali ya Jamhuri na Muungano masuala kama mahakama, dola na mengineyo yatakuwa rahisi kuyaingiza katika rasimu kwa kuzingatia mfumo utakaokuwa umekubaliwa na wajumbe wengi wa Bunge la Katiba," alisema Sitta.
Marekebisho kanuni yasitishwa Katika hatua nyingine, Bunge Maalumu la Katiba jana limesitisha azma yake ya kuwasilisha marekebisho ya kanuni kama ilivyotangazwa Ijumaa, huku Mwenyekiti Sitta akisema hatua hiyo inatokana na Watanzania kuchoka kusikia wimbo wa kanuni ukiimbwa kila siku bungeni.
"Watanzania wamechoka na mjadala wa kanuni kila siku, hivyo nimesitisha ratiba ya uwasilishaji wa marekebisho ya kanuni na badala yake sasa tutaanza kazi ya kujadili rasimu kwenye Kamati. Kama kuna mgongano wowote wa kikanuni utajitokeza huko mbele tutaangalia namna nzuri ya kuutatua," alisema Sitta.
Waendelea kukosoa 3Wajumbe mbalimbali wa Bunge Maalumu la Katiba, akiwemo NaibuKatibu Mkuu wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Nancy Mrikaria wameendelea kukosoa mfumo wa Muungano wa Serikali tatu wakisema unabeba maslahi yawatu wachache.
Akizungumza na gazeti hili jana mjini Dodoma, Mrikaria alisema wajumbe hao wameaminiwa na wananchi na wanapaswa kuangalia maslahi ya taifa na kuweka kando itikadi za kisiasa.
Aliasa wajumbe kuacha kung'ang'ania serikali tatu akisema serikali mbili bado zinafaa. "Tusiangalie serikali itakayobeba maslahi ya watu wachache, cha muhimu ni kuangalia serikali yenye maslahi ya watu wengi," alisema.
Mjumbe mwingine wa Bunge Maalumu, William Ngeleja amesema upo umuhimu wajumbe wa bunge hilo kufanya maamuzi yakuimarisha muungano na kuacha kuwa na maslahi binafsi yenye lengo la kuvunja muungano. Alisema hayo jana mjini hapa huku akisisitiza kuwa muumini wa serikali mbili.
Ngeleja alisema msingi muhimu wa rasimu ni makubaliano hivyo nimuhimu wajumbe wakafanya uamuzi utakaoimarisha muungano licha ya rasimu kutamka serikali tatu.
"Tubishane na tujadiliane kwa hoja, tunaamua hatma ya Watanzania tutimize wajibu wetu kwani wakati wa kujadili rasimu tutaangalia mambo ya kiasiasa na kisheria pia," alisema Ngeleja.
Alisema bado serikali mbili zinafaana jambo la muhimu ni kuangalia changamoto zilizopo na kupatiwa ufumbuzi badala ya kufikiria kuwa na serikali tatu. Alisema kwenye kundi la watu 600 kusitegemewe kuwa na mawazo ya aina moja.
Alisihi Watanzania kuwa na amani na utulivu. Alisisitiza kazi ya kutunga katiba ni ya wananchi wote. Alisema ni halali watu walio nje kuendelea kutoa maoni yao na misimamo tofauti kwani baadaye maoni yanachukuliwa na kuchaguliwa yale yanayofaa na yasiyofaa.
Chanzo: Habari leo