Amon Mpanju, ambaye ni mjumbe anayetoka kwenye kundi la wateule201, alisema mpaka wakati Bunge hilo linamaliza kutengeneza na kuthibitisha kanuni zake, kisheria lilikuwa limebakiwa na siku 32 tu.
Mpanju alisema hata hivyo, marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba yalitoa mamlaka kwa Rais wa Jamhuri baada ya kushauriana na kuafikiana na Rais wa Zanzibar, kuongeza muda wa Bunge hilo kufanya kazi, siyo kwa siku 20 bali kwa mujibu wa itakavyoonekana inafaa.
Ingawa hakupendekeza siku ngapi zinafaa kuongezwa, Mpanju alieleza kuwapo umuhimu wa Bunge hilo kuongezewa muda akisema muda uliyopangwa ni finyu mno.
Naye Kangi Lugola alisema ni muhimu kuongeza muda wa kazi zaBunge la Katiba ili mijadala ifanyike kiufasaha.
"Mimi naona tungeongezewa mara mbili ya muda uliopangwa awali (wa siku 70) angalau ingesaidia kufanya kazi kwa kiwango kizuri kidogo, kwa kuwa aina ya Katiba tunayofanyia kazi ni ngumu ikilinganishwa na nyingine nyingi duniani, kutokana na aina ya Muungano wetu," Lugora alieleza.
Tofauti na wajumbe hao, mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema kuongezwa muda bila utashi wa kisiasa hakutasaidia kitu.
"Hata wakiongeza muda hadi kufikia miezi sita, haitawasaidia kwa kuwa kuna kila dalili zinazothibitisha kuwa CCM ambao ni wengi na wenye dola hawako tayari na hawana utashi wa kisisasa," alisema Mbowe.