Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda Mkoa wa Katavi limepitisha uamuzi wa kuhamisha Ofisi za Makao yake makuu ya Halmashauri wilaya hiyo kutoka Mjini Mpanda na kuhamishia makao makuu yake mapya katika Tarafa ya Kabungu Wilayani
Uamuzi huo ulitolewa hivi karibuni katika kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilayani ya Mpanda kilichofanyika katika ukumbi wa Idara ya Maji kilichoongozwa na mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Yassin Kiberiti
Katika kikao hicho baadhi ya madiwani walimtaka Mwenyekiti wao wa Halmashauri hiyo awape maelezo ya kina kuhusiana nataarifa zilizoenea kuwa kuna mapendekezo yamekuwa yakitolewa kwenye vikao mbalimbali yanayopingana na uamuzi wa Baraza la Madiwani la kuhamisha ofisi za Makao yao makuu na kuhamishia Kabungu
Diwani wa Kata ya Kabungu Nassor Kasonso ndiye aliyekuwa wa kwanza kuhoji na kutaka kujua ni utaratibu upi ambao unataka kutumuka kutengua maamuzi yaliyopitishwa na Baraza la madiwani kwenye kikao chao Baraza la madiwani walioamua kuhamishia makao yao makuu Kabungu na badala yake wahamii Katuma Tarafafa ya Mwese
Mwenyekiti wa Halmashauri Yassin Kibiriti alilieleza Baraza hilo kuwa ni kweli kuna baadhi ya vikao vimekuwa vikipendekeza makao makuu yahamishiwe Kata ya Katuma bila kuwashirikisha madiwani ambao ndio wenye Halmashauri.
Aliwafafanulia maamuzi ya kikao cha Baraza la madiwani kiliisha amua makao makuu yawe Kabungu si kwinginepo labda kama baraza hilo litatengua uamuzi wao wa ambao walikuwa wameutowa hapo awali.
Baraza hilo la madiwani baada ya kupata maelezo ya mwenyekiti wao wote kwa pamoja walipitisha kwa kauli moja uamuzi wao wa kuhamishia makao yao makuu Kabungu uendelee kama ambavyo walivyokuwa wameamua toka awali na sivinginevyo.
Pia katika kikao hicho walijadili ombi la SUMA JKT ambao wameomba wapatie zaidi ya Ekari 5000 za ardhi kwa ajili ya ujenzi a kambi katika eneo la Kijiji cha Kamama Kata ya Mpanda Ndogo.
Madiwani hao walishauri kuwa kabla ya ya Halmashauri hiyo kuwapatia eneo hilo Suma JKT ni vizuri kwanza madiwani wakaenda kwenye eneo hilo na kulikaguaili kuepukana na migogoro ya ardhi ambayo inaweza kuja kujitokeza hapo baadaye.
Chanzo: Katavi Yetu