DENI LA TAIFA LAZIDI KUPAA

Mtandao wa Madenina Maendeleo Tanzania (TCDD), umebaini ongezeko la madeni ya ndani, ambayo sasa yamefikia Sh6.8 trilioni na kusababisha athari kubwa kwa jamii.

Mkurugenzi Mtendaji wa TCDD, Hebron Mwakagenda alisema hayo wakati akitoa taarifa za matokeo ya utafiti wa usimamizi wa deni la ndani.

Alisema deni hilo limeongezeka kutoka Sh811 bilioni mwaka 2002 hadi kufikia Sh6.8 trilioni Desemba mwaka 2013.

Alisema ingawa deni hilo ni dogo ikilinganishwa na deni la nje, lakini madhara yake ni makubwa kwa jamii ya Watanzania. Deni la nje kwa mujibu wa utafiti huo uliofanyika kati ya mwaka 2012-13, limefikia Sh20.2 trilioni na kwamba jumla ya deni la taifa ni Sh27 trilioni.

"Malipo ya riba kwa madeni ya ndani yamegharimu sehemu kubwaya rasilimali za Serikali katika kuyalipa ikilinganishwa na madeni ya nje," alisema.

Mwakagenda alisema asilimia 73 ya deni la ndani inatokana na benki ambazo zinatoza riba kubwa na kwamba dhamana za Serikali zimekuwa zikichangia kwa kiasi kikubwa.

Alisema hicho ni kiashiria kwamba, gharama za madeni ya ndani ni kubwa kuliko madeni ya nje ambayo yana masharti nafuu.

"Ukiangalia unaona wazi kuwa hali hiyo ni ongezeko la madeni ya ndani kwa kiasi kikubwa. Deni linaongezeka kila mwaka," alisema.

Mkurugenzi huyo alisema Serikali inatumia fedha nyingi kulipa riba zamadeni ya ndani na kusababisha kuzorota kwa huduma za jamii.

"Unaweza kuona kwamba, Serikali inatumia pesa nyingi kama riba kulipa madeni yake ya ndani," alifafanua.

Alipendekeza Serikali kuondoa misamaha ya kodi ili fedha zinazokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ziweze kutumika katika uendeshaji wa Serikali.

Taasisi hiyo ilipendekeza Serikali kuomba kibali cha Bunge kila inapotaka kukopa ili sababu za kufanya hivyo ziweze kujulikana na kusimamia utekelezaji wa fedha zinazokopwa.

Pia ilipendekeza madeni ya Serikali na taasisi zake yawekwe wazi ili vyombo vya usimamizi vipate fursaya kuyafuatilia kwa ukaribu ili kubaini maendeleo na matokeo ya madeni hayo.